AFRIKA
2 dk kusoma
WFP yadondosha chakula kutoka kwenye ndege kwa wakaazi wa Upper Nile Sudan Kusini
Usambazaji huu unaashiria ufikiaji wa kwanza wa WFP katika kipindi cha miezi minne kufikisha misaada muhimu ya chakula na lishe kwa zaidi ya watu 40,000 wanaokabiliwa na janga la njaa kwa sababu ya mizozo.
WFP yadondosha chakula kutoka kwenye ndege kwa wakaazi wa Upper Nile Sudan Kusini
WFP pia inatoa msaada kwa raia Sudan Kusini ambao wamekimbilia Gambella nchini Ethiopia / Picha: WFP EThiopia / Public domain
tokea masaa 16

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeanza kudondosha msaada wa dharura wa chakula kwa maelfu ya familia katika Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Katika eneo hili mizozo inayoongezeka tangu mwezi Machi imelazimu familia nyingi kuondoka katika makazi yao na kuzifikisha baadhi ya jamii kuwa na njaa kali.

Usambazaji huu unaashiria ufikiaji wa kwanza wa WFP katika kipindi cha miezi minne kufikisha misaada muhimu ya chakula na lishe kwa zaidi ya watu 40,000 wanaokabiliwa na janga la njaa katika maeneo ya mbali zaidi ya kaunti za Nasir na Ulang, maeneo ambayo yanaweza kufikiwa kwa ndege pekee.

"Uhusiano kati ya migogoro na njaa uko wazi sana nchini Sudan Kusini na tumeona hili katika miezi michache iliyopita katika eneo la Upper Nile," Mary-Ellen McGroarty, Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini alisema.

"Bila ya kuongezwa kwa misaada, kaunti za Nasir na Ulang ziko hatarini kukumbwa na baa la njaa. Tunahitaji haraka kupeleka chakula kwa familia hizi, na tunafanya kila tuwezalo kuwafikia wale wanaohitaji zaidi kabla hali haijakuwa mbaya zaidi."

Zaidi ya watu milioni moja kote Upper Nile wanakabiliwa na njaa kali, ikiwa ni pamoja na zaidi ya watu 32,000 ambao tayari wanakabiliwa na viwango vya Janga la njaa vya juu zaidi kutokana na uhaba wa chakula.

Idadi hii imeongezeka mara tatu tangu mzozo kati ya makundi yenye silaha ulipozuka mwezi Machi, na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao, ikiwa ni pamoja na kuvuka mpaka na kuingia Ethiopia.

Katika mji wa Gambella WFP inatoa msaada wa chakula muhimu kwa maisha ya watu wapatao 50,000 ambao wameondoka kutoka makazi yao ya Upper Nile kutafuta chakula na usalama.

WFP inalenga kuwafikia watu 470,000 katika Upper Nile na Kaskazini mwa Jonglei kipindi hiki cha njaa - ambao unaendelea hadi Agosti - lakini kuendelea kwa mapigano na vikwazo vya kuwepo kwa zana za msingi kumezuia upatikanaji na kufikia watu kama inavyotarajiwa.

WFP imeweza kufikia watu 300,000 pekee katika Upper Nile hadi sasa mwaka huu.

Njia kuu za mito kuingia jimboni lazima zifunguliwe tena kwa haraka ili kufikia familia zenye njaa kwa msaada endelevu kwa watu.

Njia hizi ndizo njia za gharama nafuu zaidi za kufikia maeneo makubwa ya Upper Nile na majimbo ya kaskazini ya Jonglei ili kutoa msaada muhimu lakini zimezuiwa na mapigano makali tangu katikati ya mwezi Aprili.

WFP ina tani 1,500 za chakula tayari kusafirishwa pale njia za mtoni zitakapoanza kufanya kazi tena.


CHANZO:TRT Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us