Afrika Kusini haiipingi Marekani na bado inahitaji kufanya majadiliano na Marekani, msemaji wa wizara ya biashara amesema, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuwa ataongeza ushuru wa asilimia 10 zaidi kwa nchi zenye ushirikiano na BRICS.
Trump alishtumu muungano huo wa BRICS wa mataifa yanayoendelea, ambao Afrika Kusini ni nchi wanachama, kwa sera za "kuipinga Marekani" siku ya Jumapili huku viongozi wa BRICS wakifanya kongamano lao nchini Brazil.
Afrika Kusini imekuwa ikijaribu kujadiliana na serikali ya Trump kufikia makubaliano ya kibiashara tangu mwezi Mei, wakati Trump alipokuwa mwenyeji wa Rais Cyril Ramaphosa katika Ikulu ya Marekani.
"Bado tunasubiri mawasiliano rasmi kutoka Marekani kuhusu makubaliano ya biashara lakini mazungumzo yetu yanaendelea vizuri na yana matumaini," msemaji wa wizara ya biashara Kaamil Alli ameliambia shirika la habari la Reuters.
‘Hatupingi Marekani’
"Kama tulivyowasiliana hapo awali, hatupingi Marekani," Alli alisema.
Trump amesema kuwa Marekani itaongeza ushuru wa asilimia 10 zaidi kwa nchi zozote zinazoshirikiana na "wanaopinga sera za Marekani" za kundi la BRICS kwa mataifa yanayoendelea, ambao viongozi wake walianza mkutano wao Brazil siku ya Jumapili.
"Nchi yoyote ambayo inajiweka karibu na BRICS ambayo sera zake ni dhidi ya Marekani, itatozwa ushuru wa asilimia 10 zaidi. Hakuna kufumba macho kuhusu sera hii. Asante kwa kunifuatilia kwa makini kuhusu suala hili!" Trump aliandika katika mtandao wa kijamii wa Truth Social.
Trump hakueleza zaidi kuhusu ujumbe huo wa "Kupinga sera za Marekani".