AFRIKA
3 dk kusoma
Ulinzi mkali waimarishwa, Kenya ikiadhimisha siku ya 'Saba Saba'
Julai 7 ya kila mwaka, raia na wanaharakati nchini hukumbuka mwaka 1990, wakati ambapo wapinzani wa rais wa wakati huo Daniel Arap Moi walipozindua azma ya kuibadilisha nchi kuwa demokrasia ya vyama vingi.
Ulinzi mkali waimarishwa, Kenya ikiadhimisha siku ya 'Saba Saba'
Jijini nairobi siku ya Saba saba imeadhimishwa chini ya ulinzi mkali / picha: Reuters
tokea masaa 16

Polisi nchini Kenya walifyatua mabomu ya kutoa machozi na kufungulia maji ya kuwasha dhidi ya waandamanaji jijini Nairobi, wakati Wakenya wakikumbuka miaka 35 ya uungaji mkono michakato ya kidemokrasia, siku ya Julai 7, 2025.

Julai 7 ya kila mwaka, raia na wanaharakati nchini hukumbuka mwaka 1990, wakati ambapo wapinzani wa rais wa wakati huo Daniel Arap Moi walipozindua azma ya kuibadilisha nchi kuwa demokrasia ya vyama vingi.

Maandamano hayo, yamepewa jina la ‘Saba ‘Saba’, yakishahibiana na tarehe na mwezi husika.

Hali ya usalama ilizidi kuimarishwa jijini Nairobi na viunga vyake, tangu kutokea kwa maandamano ya vijana wa ‘Gen Z’ ya Juni 2024, ambayo kati ya mambo mengine, yaliangazia maswala mbalimbali kama vile ufisadi, ukatili wa polisi na kutoweka kwa wakosoaji wa serikali.

Hapo awali, polisi walifunga barabara kuu zinazoingia Nairobi na kuzuia misongamano ya magari ndani ya jiji.

Shule nyingi na bishara zilifungwa kwa hofu ya kuibuka kwa vurugu.

"Hatuko tayari kurudi nyumbani kwa sababu nani atapigania haki zetu wakati huo? Tutakuwa hapa hadi jioni," Francis Waswa, mfanyakazi wa ujenzi, aliiambia Reuters.

Siku ya Saba Saba nchini Kenya ilianzia Julai 7, 1990, wakati viongozi wa upinzani Kenneth Matiba, Charles Rubia na Jaramogi Oginga Odinga walipokaidi utawala wa chama kimoja wa Rais Daniel arap Moi.

Tangu 1982, taifa la Kenya lilikuwa chini ya utawala wa chama kimoja cha KANU, wakati ambapo upinzani wa kisiasa na uhuru wa vyombo vya habari ulidhibitiwa.

Siku hiyo, viongozi wa upinzani waliitisha maandamano nchi nzima kudai marekebisho ya kisiasa.

Wahusika wakuu walikuwa pamoja na Kenneth Matiba, Charles Rubia na Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga. 

Serikali ilijibu kwa kuwakamata na kuwakandamiza waandamanaji. Maandamano hayo yalizua vuguvugu la kitaifa lililoishinikiza serikali kubatilisha Kifungu cha 2A na kurejesha demokrasia ya vyama vingi mwaka 1991. 

Tangu wakati huo, kila mwaka Wakenya wamekuwa wakiadhimisha siku hiyo kwa ajenda tofauti.

Kwa mfano, 1997 mwanasiasa Koigi wa Wamwere aliongoza maandamano ya kupinga na kukashifu matokeo ya uchaguzi. 

Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, kwa vipindi tofauti vya mwaka 1997, 2001, 2005, hadi na 2023, aliendelea kutetea huru na haki, akilaani kura za maoni dhidi ya serikali ya Moi.. 

Mnamo 2003, mwanamazingira Wangari Maathai aliongoza maandamano ya haki ya mazingira na urejeshaji wa ardhi. 

Mwaka 2003 na 2005 siku hiyo iliangazia mabadiliko ya katiba huku miaka mitatu baadaye, iliadhimishwa kwa kuwakumbuka waathirika wa mzozo baada ya uchaguzi. 

Mwaka 2013 na 2014, wanaharakati waliadhimisha kwa kupinga ukatili wa polisi na dhuluma za ardhi na mauaji ya vijana. 

Mnamo 2024, Wakenya walifanya tamasha la kuwakumbuka waliouawa kwenye maandamano ya mwaka huo. 

Mwaka huu 2025, Wakenya wanapoadhimisha siku ya Saba Saba, siku hiyo pia inakuja wakati vijana wa Gen Z wanapinga sera za Rais William Ruto tangu 2024.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us