AFRIKA
2 dk kusoma
UN inasema watu milioni 1.5 wanahitaji maji safi haraka huku Chad ikikabiliwa na matatizo
Mratibu wa masuala ya misaada ameonya kuhusu tatizo la hatari ya kipindupindu huku idadi ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Sudan ikiongezeka
UN inasema watu milioni 1.5 wanahitaji maji safi haraka huku Chad ikikabiliwa na matatizo
Watu wa Chad wamekusanyika kupata maji safi mjini N’Djamena, Chad 23 Julai, 2021. ( Sinan Balcıkoca - Anadolu Agency )
13 Juni 2025

Chad inaelekea kwenye tatizo kubwa kutokana na idadi kubwa ya watu kuingia nchini humo, huku watu milioni 1.5 wakihitaji kwa haraka maji safi na ni idadi ndogo ambayo imefanikiwa kupata huduma hiyo kufikia sasa, ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu misaada ilisema siku ya Ijumaa.

Akizungumza wakati wa mkutano wa UN na waandishi wa habari mjini Geneva, Mratibu wa masuala ya misaada kwa watu Francois Batalingaya anasema kuwa "wengi wanapata tu lita 5 za maji kwa siku, ikiwa ni kiwango kidogo ikilinganishwa na lita 15 zinazohitajika."

Tatizo la ukosefu wa maji limefanya kuwa gumu zaidi kutokana na mrundikano wa watu na mazingira yasiyo safi yanaleta hofu ya mlipuko wa kipindupindu, huku kukiwa na maambukizi eneo la kilomita 10 kutoka kwa kambi ya wakimbizi ya Adre, kulingana na mratibu huyo.

"Huu ni wito wa kutolewa kwa misaada tukishindwa kuchukua hatua sasa – kuungana pamoja, na raslimali, na dhamira – maisha ya watu yatapotea,na hali itakuwa mbaya zaidi," Batalingaya amesema.

Wakimbizi kutoka Sudan zaidi ya 850,000 wamekimbilia Chad tangu kuanza kwa vita nchini kwao, na kuongeza katika idadi ya watu 400,000 ambao tayari wako huko. Watu karibu 300,000 wamekwama mpakani, wengi wakiwa wanalala katika maeneo yasiyo na mahema, maji safi, au huduma za afya.

"Wanawasili wakiwa katika hali mbaya, njaa, na bila ya chochote," Batalingaya alisema, akiongeza kuwa wanaeleza simulizi za "mauaji ya halaiki, unyanyasaji wa kingono, na jamii nzima kuharibiwa."

Msimu wa kabla ya mavuno wa Chad pia umekuwa mbaya, anasema, huku watu milioni 3.3 wakiwa hawana uhakika wa kupata chakula mwaka huu – ikiwa ni 400% ikilinganishwa na muongo mmoja uliopita.

Umoja wa Mataifa na mashirika washirika 65 wanaomba ufadhili wa dola bilioni 1.4 ili kukabiliana na hali hiyo lakini wamepata 9.3% ya waliokuwa wanatarajia. "Tunafanya kila tunachoweza katika eneo hilo," Batalingaya alisema. "Lakini bila kupatikana kwa ufadhili, hatuwezi kutoa msaada."

Alisisitiza kuwa mzozo huo hautishii tu wakimbizi, lakini pia jamii za watu wa Chad ambazo ni wenyeji wa wakimbizi hao.


CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us