Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameamuru kuwe na usajili wa raia wa Rwanda walio nchini humo.
Hii inafuatia mkutano wake na wawakilishi wa raia hao katika Ikulu ya Entebbe 23 Juni 2025 ambapo walilamika kuwa wananyanyaswa.
Abavandimwe kama wanavyoitwa pia waliwasilisha ombi bungeni mwezi Aprili 2024 wakikemea ubaguzi na ukiukwaji wa haki zao za uraia.
Ingawa wanatambulika kama kabila la 24 la Uganda chini ya Katiba ya 1995, Jumuiya ya Wanyarwanda hao bado inakabiliwa na ubaguzi, hasa katika kupata uraia na hati za kusafiria, huku baadhi wakihojiwa kuhusu utambulisho wao wa Uganda.
Rais Museveni amesema kuwa raia Wanyarwanda wapo katika sehemu mbili, wale waliokuwa nchini humo kabla ya mipaka ya Uganda kuwekwa mwaka 1962 na wale waliokuja baada ya hiyo.
“Kile ambacho hatuwezi kukubali kwa sasa ni uraia pacha na nchi jirani zetu na nchi za Afrika,” Rais Museveni amesema huku akisisitiza usajili wa Wanarwanda hao.
“Uraia pacha kwa sasa unafaa kuwa kwa watoto wetu walioenda nchi za ulaya, uarabuni na Asia hasa kwa sababu ya ukosefu wa usalama hapa,” ameongezea katika taarifa yake.
Rais Museveni amesema usajili wa Wanyarwanda unafaa kufanywa na viongozi wa mitaa.
“Hakutakuwa na malipo wa usajili kwa wale walioingia Uganda kabla ya 1962, waliokuwa baada ya hiyo wanapswa walipe,” Rais Museveni ameongezea.
Amesema wakimbizi waliobaki baada ya wenzao kurejea nyumbani huenda wakapewa uraia baada ya mabadiliko ya kisheria.