Kwa miaka mingi katika jamii za wafugaji ni nadra kukuta wanawake wakimiliki mifugo, jambo ambalo sio tu linaonekana kama mfumo dume lakini pia ukandamizaji dhidi yao.
Lakini kila uchao mambo yanaonekana kubadilika. Kwa mfano, kaskazini magharibi mwa Tanzania, kikundi cha wanawake takriban 20 wakiwa na wanaume, wameanzisha kikundi kiitwacho Rotijengwa ambacho huimba nyimbo za asili kuihamasisha Serikali kupeleka huduma ya kutibu mifugo yao.
Miongoni mwa wanakikundi hao ni Ruewish Mashauri Kisumunda, mfugaji na mkazi wa kijiji cha Sarakwa Wilayani Bunda Mkoani Mara.
Mwandishi wa makala hii alimtembelea nyumbani kwake na kumkuta akiandaa maziwa kienyeji kwa ajili ya mafuta ya samli na mengine kwa ajili ya watoto.
Mashauri anadai kuwa, licha ya kuwa ni mfugaji wenye uzoefu wa miaka mingi, mavuno yamekuwa duni, hivyo ameshindwa kufaidika na matunda yatokanyo na mifugo, ikiwemo maziwa, nyama na wakati mwengine hata mauzo ya hasara kwa mifugo.
“Nililisha mifugo majani kama tiba, lakini ukiamka asubuhi unakuta kondoo wamekufa. Nilikuwa naumia sana na kujiona masikini,” anaelezea.
“Nilikuwa namiliki kondoo hamsini, na ng’ombe mia moja lakini baada ya mwaka nikajikuta nimebaki na na kondoo wawili,” ameongeza.
Mashauri sasa ni miongoni mwa maelfu ya wafugaji wanaonufaika na chanjo inayoendelea kutolewa kwa ufadhili wa Serikali ya nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.
Kwa mujibu wa serikali, dhamira yake ni kulinda mifugo na wafugaji ili wawe na ufugaji wa uhakika utakaowawezesha kukopesheka katika taasisi za kifedha ikiwemo mabenki.
Hata hivyo, katika ziara yake ndani ya mikoa sita ya Tanzania, Dkt. Ashatu Kijaji ambaye ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi ameendelea kusitiza umuhimu wa wafugaji kuitikia mwito wa Serikali ya kupeleka mifugo kupata chanjo na kuvishwa herene za kielektroniki.
“Wafugaji tunakwenda kunufaika, lakini ombi langu kwenu na shauku ya Rais Samia ni mifugo yenu kupatiwa chanjo,” amesema Kijaji.
“Sisi tumejitoa kutunga wimbo kufikisha kilio chetu Serikalini na natabasamu kwa furaha,” nilikata tamaa ya kufuga kabisa,” anasema Anna Mahega mmoja wa wanakikundi na kuongeza, “Serikali imesikia kilio chetu.”
Miongoni mwa changamoto ya miaka mingi kwa wafugaji ni pamoja na mifugo yao kuugua ugonjwa wa tauni maarufu (Sotoka) au homa ya mapafu.
“Nilipoona mifugo yangu imelewa, nililazimika kuponda matawi ya miti kama dawa ya kienyeji, ambayo pia hakuna uhakika wa kuponyesha mifugo, nilipoteza watoto 15 wa kondoo kwa siku moja kwa sababu ya magonjwa hayo, lakini leo tumepata chanjo salama,” amesema.
Ikiwa zoezi hili halitopata mkwamo, malengo ya serikali ni kuchanja ng’ombe milioni 19, mbuzi na kondoo milioni 17 na kuku milioni 40 ifikapo 2030.