Afrika yapambana na ukosefu wa chanjo ya Mpox, ugonjwa wa kipindupindu ukiongezeka
MAISHA
5 dk kusoma
Afrika yapambana na ukosefu wa chanjo ya Mpox, ugonjwa wa kipindupindu ukiongezekaHadi kufikia mwezi Julai 2025, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kilikuwa kimerekodi maambukizi 25,175 kutoka mataifa 23.
Kuna chanjo ya kuwakinga watu dhidi ya Ugonjwa wa Mpox / picha: Reuters
4 Julai 2025

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kimeonesha hofu kubwa kuhusu kutokea kwa milipuko mipya minee ya magonjwa ya Kipindupindu, Homa ya Dengue, Mpox na Surua.

Kulingana na Africa CDC, maambukizi ya Mpox yanapungua, japo bara la Afrika linashindwa kutoa chanjo kwa nchi wanachama kutokana na uhaba wa fedha.

"Chanjo zinaendelea kutolewa ingawa tunafikia mahali tunaishiwa kabisa na kushindwa kusambaza kwa nchi husika. Nchi 6 tayari zinasubiri chanjo. Lakini hazipatikani. Kwa hiyo hii ni changamoto kubwa ambayo tunapaswa kutatua," anaelezea Dkt. Yap Boum, Naibu Meneja wa kupambana na ugonjwa wa Mpox ndani ya Africa CDC.

Nchi hizo ni pamoja na Ethiopia, Malawi, Tanzania, Ghana, Sudan Kusini, na Guinea.

Hadi kufikia mwezi Julai 2025, Africa CDC ilikuwa imerekodi maambukizi 25,175 kutoka mataifa 23.Watu 574 wameripotiwa kufa kwa Mpox barani hadi sasa.

Takwimu kutoka kwa taasisi hiyo zinaonesha kuwa, tayari dozi milioni 3 za chanjo zimesambazwa barani Afrika.

Wakati huo huo, mataifa 11 yamepata chanjo hiyo, huku saba kati hayo yakiendelea kuchanja raia wake.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) linaripoti kuwa linahitaji kupata kupata ufadhili wa dola milioni 33 kununua dozi 500,000 za chanjo ya Mpox kwa ajili ya kusambazwa kwa nchi zenye mahitaji.

"Hatuna uwezo kama bara wa kukabiliana na matibabu, ikiwa ni pamoja na chanjo,” anasema Dkt. Mercy Kyeng, Kiongozi wa Kitengo cha Utafiti wa magonjwa katika taasisi ya Afrika CDC.

"Kwa kweli tunatetea nafasi hiyo na ajenda ya utengenezaji wa chanjo ya ndani na hata uchunguzi mwingine," anaongeza.

Mafanikio katika chanjo ya Mpox

Uhaba wa chanjo ya Mpox unakuja wakati baadhi ya nchi zimethibitisha mafanikio katika kudhibiti ugonjwa huo kupitia chanjo.

"Uganda imepokea dozi 97,000 hivi karibuni, na wametumia asilimia 96 ya dozi 100,000 ambayo wamepokea hapo awali kwa mbinu iliyolengwa ya chanjo ambayo wamekuwa wakitumia," anaeleza Dkt. Boum kutoka Afrika CDC.

"Kwa hivyo kipimo watakachopokea kitakuwa sehemu ya awamu inayofuata, na watazingatia sehemu kubwa iliyobaki ili kuhakikisha kuwa kwa hizo dozi 100,000 wanaweza kuwa na na pia kutathmini ufanisi wa chanjo," anaongeza.

Kwa upande mwingine, Sierra Leone iko katika awamu ya tatu ya kampeni kuhakikisha kwamba wanachanja watu 70,000 kwa siku 10.

"Ndio chanjo zinapatikana katika kiwango cha mtengenezaji, lakini ufadhili wa kuzipata ndio shida,” Dkt. Boum anabainisha.

Kuongezeka kwa kipindupindu

Kipindupindu bado ni changamoto kubwa ya kiafya kwa bara hilo la Afrika, huku taasisi ya Africa ikianisha mlipuko wa ugonjwa katika nchi 21 hadi sasa.

Hadi kufikia Juni 2025, kulikuwepo na mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi kadhaa kama vile DRC, Sudan, Sudan Kusini na Angola.

"Changamoto ya Kivu Kusini ni ukosefu wa maji safi ya kutosha," anaeleza.

Ugonjwa huo hata hivyo, umeenea katika maeneo mengine ni pamoja na Kivu Kaskazini, Haut Katanga, Haut Lomami na Tanganyika.

Vivyo hivyo, milipuko kadhaa pia imeshuhudiwa katika mji mkuu wa Kinshasa.

"Changamoto kubwa ya Kinshasa ni msongamano mkubwa wa watu na ukweli kwamba Kinshasa imezungukwa na mito tofauti ambapo watu wanapata maji, na hiyo ndiyo inayosababisha kuzuka kwa kipindupindu," anaongeza.

DRC itatekeleza chanjo ya kipindupindu katika maeneo 11 ya afya mjini Kinshasa.

Nchi nyingine ambazo zimeshuhudia mlipuko wa kipindupindu ni pamoja na Angola, Burundi, Comoro , DRC , Ethiopia , Ghana,  Cote d'Ivoire,  Kenya, Malawi , Msumbiji Namibia.

Pia zipo Nigeria, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania, Togo, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Uzalishaji wa chanjo Afrika

Baada ya changamoto kubwa ya upatikanaji wa chanjo kushuhudiwa zaidi wakati wa janga la Uviko 19, wakuu wa nchi za Afrika walikubaliana kuharakisha utengenezaji wa chanjo barani Afrika kwa Afrika.

Wakati wa mkutano wao wa mwaka 2024, viongozi hao waliamua kuanzisha Utaratibu wa Ununuzi wa Pamoja (PPM) kwa msaada wa Afreximbank na Tume za Kiuchumi za Umoja wa Mataifa kwa Afrika ili kuboresha uwezo wa kumudu, upatikanaji wa vifaa vya matibabu vya ubora wa juu katika bara zima.

Mpango wa Kuharakisha Utengezaji wa Chanjo barani Afrika (AVMA), wenye kugharimu Dola Bilioni 1.2 ulizinduliwa Juni 2024.

Utaratibu wa miaka 10, unalenga kuharakisha upanuzi wa utengenezaji wa chanjo zinazofaa kibiashara barani Afrika.

Aidha, Afreximbank ilizindua ahadi ya Dola Bilioni 2 kusaidia Utengenezaji wa Bidhaa za Afya za Kiafrika mnamo 2024. Utafiti uliofanywa na CDC ya Afrika na matokeo yake kutolewa Oktoba 2024, ulionesha kuwa kufikia Juni 2024, kulikuwa na miradi 25 inayoendeshwa katika bara zima.

Hivi sasa, uwezo uliosakinishwa wa chanjo inakadiriwa kuwa dozi bilioni 1.4 kufikia 2030, ambayo utafiti wa Africa CDC unaonyesha inaweza kuongezeka hadi dozi bilioni 2 kila mwaka katika hali za dharura.

Ikiwa miradi mingi itapatikana, uwezo huo utaboreka tu.

Afrika CDC hata hivyo, ina wasiwasi kwamba ingawa Afrika ina matarajio na njia nyingi za kufikia malengo yake ya uzalishaji wa chanjo, bado haina uhakika wa mahitaji na kesi thabiti ya biashara kuendeleza azma hiyo.

"Mipango inaonesha kuwa kati ya 2025 na 2030, wazalishaji watatu wa chanjo barani Afrika wanatarajiwa kuzalisha na kupata mahitaji ya awali ya Shirika la Afya Duniani kwa chanjo tisa tofauti. Hata hivyo mahitaji ya sasa ya soko ya chanjo hizi bado hayana uhakika," utafiti unaeleza.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us