China siku ya Jumatatu imejibu vitisho vya ushuru wa "ziada" wa Marekani kwa mataifa "yanayoshirikiana" na BRICS, ikisema "hakuna washindi" katika vita vya biashara.
"Tunaamini BRICS ni nguvu ya manufaa katika jumuiya ya kimataifa na hailengi mhusika wa tatu," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning aliambia mkutano wa habari uliorushwa moja kwa moja mjini Beijing.
Katikati ya mkutano unaoendelea wa viongozi wa jumuiya ya BRICS nchini Brazil, Rais wa Marekani Donald Trump alionya siku ya Jumapili kwamba nchi yoyote ambayo inajifungamanisha "na sera za kupinga Marekani" za jumuiya ya kiuchumi ya BRICS itakabiliwa na ushuru wa ziada wa 10%.
"Ushuru huu utatakelezewa kwa kila mtu bila ya kubagua," aliandika kwenye jukwaa lake la ‘Truth Social’.
Mfumo mbadala wa kifedha
Hata hivyo, Mao alisema China "siku zote inapinga vita vya ushuru na vita vya kibiashara... Tunapinga matumizi ya ushuru kama chombo cha kulazimisha na kushinikiza wengine. Uwekaji ushuru haumfaidishi mtu yeyote."
"BRICS ni jukwaa muhimu la ushirikiano kati ya masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea. Inatetea ushirikishwaji na ushirikiano wa kumfaidi kila mtu," Mao aliongeza.
BRICS ilianzishwa mwaka 2009 na Brazil, Urusi, India na China, huku Afrika Kusini ikijiunga mwaka 2010.
Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ethiopia, Indonesia, na Iran baadaye zilijiunga na kupanua kundi hilo hadi wanachama 11, sambamba na nchi 10 washirika wa kimkakati.
Muungano huo unalenga kuunda mifumo mbadala ya kifedha, kupunguza utegemezi wa dola, na kuongeza uwakilishi wa Kimataifa wa Kusini katika taasisi za kimataifa, kutoa changamoto kwa miundo ya utawala inayoongozwa na Magharibi.