Masoko ya hisa ya dunia yalishuka siku ya Ijumaa na bei ya mafuta ilipanda wakati Israel ilipoanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, na kusababisha watu na wawekezaji kukimbilia katika uwekezaji salama kama vile dhahabu, dola na faranga ya Uswizi.
Kuongezeka kwa mzozo Mashariki ya Kati - eneo kubwa linalozalisha mafuta - kunaongeza kutokuwa na uhakika kwa masoko ya fedha wakati wa shinikizo kubwa kwa uchumi wa dunia kutoka kwa sera za biashara za Rais wa Marekani Donald Trump.
Mapema Ijumaa Trump aliitaka Iran kufanya makubaliano juu ya mpango wake wa nyuklia, akisema kwamba bado kuna wakati kwa nchi hiyo kuzuia mzozo zaidi na Israeli.
Mwitikio wa soko, ambao ulikuwa umepungua katika biashara ya mapema ya Ulaya, ulipanda kwa kasi mpya wakati kikao kikiendelea.
"Ni wazi suali kubwa ni kwamba hii itaenda umbali gani?," alisema Chris Scicluna, mkuu wa utafiti wa kiuchumi katika Masoko ya Mitaji ya Daiwa huko London, akimaanisha mvutano wa Mashariki ya Kati.
"Soko lilikuwa linaendelea vizuri kwa suala la hisa ya chini na bei ya chini ya mafuta na dhahabu."
Bei ya mafuta yasiyosafishwa ya Brent ilipanda kwa karibu asilimia 9 kwa $75.54 kwa pipa kuweka historia ya kupanda kwa bei kwa kasi hiyo kwa siku moja tangu 2022, wakati gharama ya nishati iliongezeka baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Athari kwa Afrika
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika amekashifu mzozo kati ya Israeli na Iran akiomba uhasama usitishwe.

Maendeleo hayo ya mzozo yanamaanisha hatari nyingine kubwa ya kijiografia na kisiasa ambayo lazima yataathiri Afrika.
Bei ya dhahabu nayo ambayo ni rasilimali salama ya uwekezaji nyakati za kutokuwa na uhakika duniani, ilipanda kwa 1% hadi $3,416 kwa wakia, na kuisogeza karibu na rekodi ya juu ya $3,500.05 kuanzia Aprili.
Ni wakati mzuri sasa kwa nchi zinazozalisha dhahabu kama Afrika Kusini na Tanzania kupata mauzo mazuri ya madini haya.
Kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, ambapo asilimia 17 ya uzalishaji wa mafuta duniani hutiririka, kunaweza kuathiri bei ya nishati duniani kwa kiasi kikubwa.
Hormuz iko kati ya Oman na Iran, inaunganisha Ghuba ya Persia na Ghuba ya Oman na Bahari ya Arabia. Mlango huo ni njia muhimu ya kusafirisha mafuta ghafi duniani kila siku.
Wataalamu wanasema wazalishaji mafuta Afrika kama Angola, Gabon na Nigeria wana fursa ya kuchuma kipato cha juu kwa mauzo ya mafuta yao.
Usafiri wa anga kuathiriwa
Hata hivyo, bei ya mafuta ya ndege huenda ikaongezeka kwa sababu ya mzozo huu na kukatika kwa mtiririko wa kawaida wa mafuta.
Kuongezeka kwa gharama za mafuta kwa mashirika ya ndege na usafirishaji wa anga na hivyo kuongeza bei kwa watumiaji.
Wasafiri pia wanaotarajia kuelekea maeneo yanayoathriiwa, itabidi waahirishe safari zao.
Shirika la Ndege la Kitaifa la Israel, El Al Airlines, lilitangaza kusimamisha safari zake za kwenda na kutoka Israel.
Ndege kadhaa za kibiashara kutoka mashirika kama Emirates ya Dubai, Lufthansa, na Air India zilikuwa zikisafiri juu ya anga ya Iran.
Air India, ambayo hutumia anga ya Iran kwa safari zake za Ulaya na Amerika Kaskazini, ilisema safari kadhaa zilibadilishwa au kurudishwa zilipotoka, zikiwemo zile kutoka New York, Vancouver, Chicago, na London.
Uhusiano wa kidiplomasia
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa ya Afrika na Iran au Israel pia unaweza kubadilika kutokana na mzozo huo.
Baadhi ya nchi za Kiafrika hudumisha uhusiano thabiti na Israel, mara nyingi kutokana na ushirikiano wa kiuchumi, kiteknolojia au kijeshi.
Iran inapojaribu kupanua ushawishi wake, mataifa haya yanaweza kuhisi shinikizo kutathmini upya miungano yao.
Kwa mfano, nchi za Afrika Mashariki ambazo zimeanzisha uhusiano na Israeli kwa ajili ya maendeleo ya kilimo na teknolojia zinaweza kujikuta zikipitia mazingira magumu ya kidiplomasia, hasa kama zinakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wahusika wengine wa kikanda wanaofungamana na Iran.