MICHEZO
3 dk kusoma
CHAN 2024: Wenyeji Tanzania waichabanga Burkina Faso katika mechi ya ufunguzi
Mwenyeji Tanzania wameanza kampeni yao ya CHAN kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Burkina Faso baada ya sherehe za ufunguzi.
CHAN 2024: Wenyeji Tanzania waichabanga Burkina Faso katika mechi ya ufunguzi
Tanzania iliifunga Burkina Faso katika mchezo wa kwanza wa CHAN 2024 Jumamosi, Agosti 2. Picha: TFF/X
3 Agosti 2025

Taifa Stars ya Tanzania imepata ushindi wake wa kwanza kabisa katika mechi ya ufunguzi ya CHAN, baada ya kuifunga Burkina Faso 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Abdul Sopu alifungua ukurasa wa ushindi kwa mkwaju wa penalti uliopigwa kwa utulivu katika kipindi cha kwanza, baada ya Clement Mzize kufanyiwa madhambi na Frank Tologo. Beki Mohamed Hussein alihakikisha ushindi kwa kichwa kizito katikati ya kipindi cha pili, jambo lililowafanya mashabiki wa nyumbani kufurahia kwa shangwe kubwa.

Ushindi huu unaiweka Tanzania katika nafasi nzuri mapema kwenye Kundi B, ambalo pia linajumuisha Burundi na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Burkina Faso bado inaendelea kusubiri ushindi wa kwanza katika mechi za ufunguzi za CHAN, baada ya kushindwa katika mara nne za kwanza walizoshiriki.

Mechi ilianza kwa kasi, huku timu zote mbili zikijaribu kutengeneza nafasi, lakini wenyeji walitawala sehemu kubwa ya mchezo. Clement Mzize na Feisal Salum wa Tanzania walimjaribu kipa wa Burkina Faso, Ladji Sanou, mapema, huku Yakoub Suleiman akifanya kazi ya ziada kuzuia nafasi za Souleymane Sangaré na Papus Ouattara.

Baada ya mapumziko, Burkina Faso ilifanya mabadiliko matatu, ikiwaleta wachezaji wazoefu kama Patrick Malo na Yves Koutiama. Hata hivyo, Tanzania iliendelea kushambulia, na kichwa cha Mohamed Hussein kutoka kwa mpira wa kona wa Mudathir Yahya kilihakikisha ushindi.

Burkina Faso ilijaribu kushambulia kwa nguvu katika dakika 10 za mwisho, lakini ilikosa utulivu mbele ya lango, huku mashuti ya Tertius Bagré na Ouattara yakipaa nje. Taifa Stars walidhibiti hali na kupata alama zote tatu, wakitarajia kuendeleza kasi hii katika mechi yao inayofuata ya kundi kwenye mashindano ya CHAN 2024.

Mechi hii ilifanyika baada ya sherehe ya ufunguzi iliyohudhuriwa na maelfu ya mashabiki na viongozi, wakiwemo viongozi wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), akiwemo rais wake Patrice Motsepe.

Mashindano haya ya CHAN, ambayo yanahusisha wachezaji wa klabu za ndani pekee, yanaandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya, na Uganda. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi hizi tatu za Afrika Mashariki kushirikiana kuandaa mashindano ya CAF tangu mwaka 1976, na pia ni mara ya kwanza kwa mashindano haya kuandaliwa kwa pamoja na nchi tatu.

Mashindano ya CHAN, ambayo yataendelea hadi Agosti 30, yanachukuliwa kama maandalizi ya mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2027, ambayo pia yataandaliwa kwa pamoja na nchi hizi tatu.

Kuandaa viwanja vitano kwa ajili ya mashindano haya kulikuwa changamoto, na CAF ililazimika kuahirisha mashindano haya kutoka tarehe iliyopangwa awali mwezi Februari ili kutoa muda zaidi wa maandalizi.

Katika ziara ya mwisho ya ukaguzi jijini Nairobi wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa CAF, Veron Mosengo-Omba, alisifu maendeleo na ushirikiano wa nchi hizi tatu. "Nadhani Afrika inapaswa kujifunza kutoka kwa mfano huu. Nchi tatu zimeunganisha juhudi na rasilimali zao kufanikisha hili," aliwaambia waandishi wa habari.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us