Uja uzito mara nyingi huja na changamoto nyingi ikiwemo maumivu na maradhi ya asubuhi, kichefuchefu, maumivu ya mgongo, uchovu na wakati mwingine maradhi hatari kama kuvuja damu au kukosa damu ya kutosha mwilini na kadhalika.
Lakini kuna baadhi ya wanawake, ambao wanapata hamu ya kula vitu visivyoeleweka. Yaani atatamani kula jiwe, mchanga, mipira ya tairi au wengine watake kula embe bichi zaidi au pilipili.
Haya yote yanafumbiwa jicho na jamii au kuchukuliwa kitu cha kawaida kwa akina mama waja wazito. Lakini unajua kuwa hii inaweza kuwa dalili ya upungufu wa madini fulani mwilini?
Matamaniio haya, japo ni kawaida kwa wanawake waja wazito, huwaathiri pia watoto wachanga na watu wengine walio na upungufu wa madini hayo.
Bumba, Udongo unaoliwa Uganda
Sally Miremba ana uja uzito wa miezi saba na kila mchana ankwenda sokoni kununua ‘bumba’. Huu ni udongo uliokaushwa na kuvunjwa vipande vidogo kuuzwa sokoni. Jina linatofautiana kulingana na nchi au eneo.
‘‘Mimi hula bumba ili inisaidie kuondoa kichefuchefu, na niache kutema mate ila wakati,’’ anasema.
Tamaa ya kula vitu hivi ambavyo sio chakula hujulikana kisayansi kama PICA. Hali hii inawaathiri watu wa kila tabaka na kila eneo duniani.
Wataalamu wa lishe wanaielezea kama upungufu wa madini mwiilini hasa ya chuma, Zinc na magnesium ambayo humfanya mtu kuingiwa na hamu hiyo.
Hatari za kula Bumba na vitu vingine visivyo chakula
Madaktari wameonya kuwa japo ulaji wa vitu hivi unakuridhisha kwa muda, unaweza kuwa na athari kubwa kwa afya yako.
Miongoni mwa athari za haraka ni utapiamlo, ukosefu wa hamu ya kula, kuvimbiwa, sumu kutoka kwa madini hatari na vyuma kama vile risasi na zebaki.
Kula vitu visivyo chakula kunaweza kutatiza ufyonzwaji wa virutubishi wa vitu vyenye afya na kusababisha upungufu. Tamaa ya Pica pia inatia wasiwasi kwa sababu vitu visivyo chakula vinaweza kuwa na viambato vya sumu au vimelea na minyoo.
Baadhi ya tafiti kwa mama waja wazito, zimeonyesha miongoni mwa athari kwa watoto ni uhusiano wa karibu sana na ulemavu wa akili, magonjwa maalum.
Madaktari wanashauri kuwa, ikiwa unaona hamu ya vitu visivyo chakula, ni bora kupata ushauri wa daktari wako haraka iwezekanavyo, ili kujua chanzo.