Marekani na Rwanda zimekubaliana nchi hiyo ya Kiafrika kuwapokea wahamiaji 250 waliofukuzwa kutoka Marekani, msemaji wa serikali ya Rwanda na afisa mmoja aliliambia shirika la habari la Reuters, huku utawala wa Rais Donald Trump ukichukua mkondo mkali kuhusu uhamiaji.
Mkataba huo, ulitiwa saini na maafisa wa Marekani na Rwanda mjini Kigali mwezi Juni, alisema afisa huyo wa Rwanda, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, akiongeza kuwa Washington tayari imetuma orodha ya awali ya watu 10 kuchunguzwa.
"Rwanda imekubaliana na Marekani kupokea hadi wahamiaji 250, kwa kiasi fulani kwa sababu karibu kila familia ya Rwanda imepitia magumu ya kuhama, na maadili yetu ya kijamii yamejengwa katika kuunganishwa na urekebishaji," alisema msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo.
"Chini ya makubaliano hayo, Rwanda ina uwezo wa kuidhinisha kila mtu aliyependekezwa kwa ajili ya makazi mapya.
Shaka juu ya haki za msingi za kibinadamu
Wale walioidhinishwa watapewa mafunzo ya wafanyakazi, huduma za afya, na msaada wa malazi ili kuharakisha maisha yao nchini Rwanda, na kuwapa fursa ya kuchangia moja ya uchumi unaokua kwa kasi zaidi duniani katika muongo mmoja uliopita."
Ikulu ya White House na Idara ya uhamiaji haikuwa na maoni ya haraka.
Rais Donald Trump analenga kuwafurusha mamilioni ya wahamiaji nchini Marekani kinyume cha sheria na utawala wake umetaka kuongeza uondoaji wa wahamiaji katika nchi za tatu, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka wahalifu waliopatikana na hatia nchini Sudan Kusini na Eswatini, ambayo zamani ilijulikana kama Swaziland.
Rwanda katika miaka ya hivi karibuni imejiweka kwenye nafasi ya kuwa nchi ya marudio ya wahamiaji ambayo nchi za Magharibi zingependa kuwaondoa, licha ya wasiwasi wa makundi ya kutetea haki za binadamu kwamba Kigali haiheshimu haki za msingi za binadamu.
Changamoto za kuhamishiwa nchi ya tatu
Mwezi Mei, waziri wa mambo ya nje alisema Rwanda ilikuwa katika hatua za awali za mazungumzo ya kupokea wahamiaji waliofukuzwa kutoka Marekani.
Utawala wa Trump unasema kuwa kufukuzwa kwa nchi ya tatu kunasaidia kuwaondoa haraka wahamiaji wengine, pamoja na wale walio na hatia ya uhalifu.
Watu wenye msimamo mkali wa uhamiaji wanaona kuondolewa katika nchi ya tatu kama njia ya kukabiliana na wahalifu ambao hawawezi kufukuzwa kwa urahisi na wanaweza kuwa tishio kwa umma.
Lakini wanaopinga wamekosoa uhamishwaji huo kuwa hatari na ukatili, kwani watu wanaweza kutumwa katika nchi ambazo wanaweza kukabiliwa na ghasia, hawana uhusiano na hawazungumzi lugha hiyo.
Rwanda kupokea ruzuku
Rwanda italipwa na Marekani kwa njia ya ruzuku, afisa huyo alisema, akiongeza kuwa barua ya ruzuku hiyo ilikamilishwa mwezi Julai.
Afisa huyo alikataa kusema ni kiasi gani cha ruzuku hiyo.
Marekani na Rwanda zinaweza kurefusha mkataba huo zaidi ya watu 250 kwa maelewano, afisa huyo alisema, akiongeza kuwa wale waliopelekwa Rwanda si lazima wabaki nchini humo na wanaweza kuondoka wakati wowote wapendao.
Kigali itakubali tu wale ambao vifungo vyao vimekamilika au ambao hawana kesi ya jinai dhidi yao, kwani hakuna makubaliano na Washington ambayo yataruhusu watu kutumikia kifungo chao cha Amerika nchini Rwanda, afisa huyo alisema.
Uhamishwaji bila kuzingatia maridhio
Rwanda pia imesema haitawapokea wahalifu wa ngono dhidi ya watoto.
Utawala wa Trump umeshinikiza nchi zingine kuchukua wahamiaji.
Iliwafurusha raia wa Venezuela zaidi ya 200 wanaotuhumiwa kuwa wanachama wa genge hadi El Salvador mwezi Machi, ambapo walifungwa jela hadi walipoachiliwa kwa kubadilishana wafungwa mwezi uliopita.
Mahakama ya Juu mnamo Juni iliruhusu utawala wa Trump kuwafukuza wahamiaji hadi nchi za tatu bila kuwapa nafasi ya kuonyesha wanaweza kudhurika. Lakini uhalali wa uondoaji huo unapingwa katika kesi ya kitaifa huko Boston, kesi ambayo inaweza kurudi kwenye mahakama kuu inayoegemea kihafidhina.
Changamoto za kisheria
Makubaliano ya kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa kutoka Marekani sio makubaliano ya kwanza kama hayo Rwanda kufikia.
Kigali ilitia saini makubaliano na Uingereza mwaka 2022 kuchukua maelfu ya watu wanaotafuta hifadhi, mkataba ambao ulitupiliwa mbali mwaka jana na Waziri Mkuu mteule wa wakati huo Keir Starmer.
Hakuna aliyetumwa Rwanda chini ya mpango huo kwa sababu ya miaka mingi ya changamoto za kisheria.