AFRIKA
1 dk kusoma
Kiongozi wa upinzani Uganda Kizza Besigye na msaidizi wake wanyimwa dhamana
Mahakama nchini Uganda imemnyima dhamana mwanasiasa Dkt. Kizza Besigye na msaidizi wake Hajj Obeid Lutale ikisema kuwa huenda wakatatiza mchakato wa uchunguzi unaoendelea
Kiongozi wa upinzani Uganda Kizza Besigye na msaidizi wake wanyimwa dhamana
Kiongozi wa upinzani Uganda Kizza Besigye / REUTERS
11 Aprili 2025

Besigye amekuwa gerezani kwa takriban miezi mitano tangu kukamatwa kwake jijini Nairobi, mwezi Novemba.

Mahakama ilijiridhisha kuwa wadhamini walikuwa watu sahihi na kwamba walikidhi vigezo vilivyotakiwa. Lakini Jaji Rosette Comfort Kania alikataa kuwaachilia kwa dhamana wawili hao akitaja uzito wa mashtaka na hasa kutokana na kuendelea kwa uchunguzi.

‘‘Uhalifu huu unadaiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini Uganda na mataifa mengine, kwa hiyo itachukuwa muda kukamilisha uchunguzi ambavyo ni tofauti na uhalifu ambao umefanyika Uganda pekee’’, Jaji Kania alisema katika maamuzi yake yaliyosomwa na msajili Ssalmu Ngoobi.

Kulingana na upande wa mashtaka, Dkt. Besigye, Hajj Lutale, Kapteni Denis Oola, na wengine ambao hawajulikani waliko wanadaiwa kupanga njama ya kupindua serikali kwa kutumia silaha kati ya 2023 na Novemba 2024.

Njama hiyo inadaiwa kupangwa katika nchi kadhaa ikiwemo Uswizi, Ugiriki, Kenya na Uganda.

Wanaomuunga mkono Besigye na ambao walikuwa wamefika katika mahakama jijini Kampala waliimba nyimbo za matumaini wakisema

“Hili litapita, hili litapita, tunaamini siku moja hili litapita,” waliimba kwa pamoja, huku wakinyoosha mikono yao kama ishara ya ushirikiano kwa kiongozi huyo wa upinzani.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us