AFRIKA
2 dk kusoma
UN yaonya ya kwamba mafuriko makubwa Sudan Kusini yanaweza kuathiri zaidi ya watu milioni 1
Mapigano, maradhi ya kipindupindu, na kupunguzwa kwa ufadhili imeongeza ukali wa janga hilo, asema mwakilishi wa shirikia la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini humo.
UN yaonya ya kwamba mafuriko makubwa Sudan Kusini yanaweza kuathiri zaidi ya watu milioni 1
Takribani watu 100,000 wamelazimika kuhama makazi yao kulingana na Marie-Helene Verney, mwakilishi wa UNHCR Sudan Kusini./ / AA
tokea masaa 7

Mafuriko nchini Sudan Kusini tayari yameathiri watu wapatao 273,000 mwaka huu, na huenda yakaathiri zaidi ya watu milioni 1 katika miezi ijayo, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) siku ya Ijumaa.

“Sudan Kusini inakumbwa tena na mafuriko makubwa sana, na kwa bahati mbaya, hasa katika maeneo ambayo tayari yameathiriwa na mapigano mapya katika kipindi cha miezi sita iliyopita,” alisema Marie-Helene Verney, mwakilishi wa UNHCR nchini Sudan Kusini, katika mkutano na waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Verney alisema idadi ya watu walioathirika imeongezeka mara tatu zaidi ndani ya mwezi Agosti pekee, huku takribani watu 100,000 wakilazimika kuhama makazi yao.

“Ikiwa hali hii itaendelea, tunakadiria kuwa zaidi ya watu milioni moja wataathirika katika miezi michache ijayo, ambapo takriban 400,000 watahamishwa,” alisisitiza, akiongeza kuwa mvua za mwaka huu ni kubwa kuliko zile za mwaka uliopita.

Verney alibainisha kuwa maeneo yote ya majimbo ya Jonglei na Unity yamejaa maji, ikiwa ni pamoja na mashamba, mifugo, nyumba, shule na vituo vya afya.

Aliongeza kuwa mafuriko hayo yanatokea wakati ambapo kuna mapigano, uhaba wa chakula, na mlipuko wa kipindupindu ambao tayari umeathiri watu wapatao 90,000.

UNHCR inalenga kutoa msaada kwa hadi watu 150,000, alisema, na msaada huo unajumuisha pesa taslimu, makazi ya dharura, bidhaa za misaada kwa waliopoteza makazi, na huduma za ulinzi.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us