Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani walifanya mazungumzo kwa njia ya simu kujadili shambulio la Israel dhidi ya ujumbe wa wapatanishi wa Hamas mjini Doha, ofisi ya Erdogan imesema.
Pia walibadilishana maoni kuhusu hatua za pamoja zinazoweza kuchukuliwa kama jibu.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Erdogan alitoa salamu za rambirambi kwa mashahidi na kusisitiza kuwa Ankara itasimama na kuunga mkono taifa na wananchi wa Qatar kwa kila namna.
Rais wa Uturuki pia alilaani shambulio la Israel kupitia taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa la kijamii wa Uturuki, NSosyal, siku ya Jumanne, akilitaja kama “uvunjifu wa wazi wa sheria za kimataifa” dhidi ya “taifa ndugu.”
“Shambulio la Israel dhidi ya ujumbe wa wapatanishi wa Hamas nchini Qatar limethibitisha wazi upofu wa hasira wa serikali ya (Benjamin) Netanyahu na dhamira yake ya kuzidisha mzozo na hali ya kutojiamini,” Erdogan alisema, akiongeza kuwa wale waliogeuza ugaidi kuwa sera ya kiserikali hawatafanikiwa.
“Kwa kukabiliana na ujambazi huu wa kigaidi wa Israel, unaolenga kujipeleka yenyewe na kanda yote katika janga, tutadumisha msimamo wetu thabiti na wa ujasiri; na bila kujali gharama yoyote, tutaendelea kutetea amani, sheria za kimataifa na uhuru wa watu wa Palestina.”
Baada ya mashambulizi hayo, Ubalozi wa Uturuki mjini Doha ulisema unafuatilia kwa karibu matukio hayo, ukihimiza raia wa Uturuki kufuatilia kwa makini matangazo kutoka kwa mamlaka za Qatar, pamoja na yale yatakayochapishwa kupitia akaunti rasmi za mitandao ya kijamii na tovuti ya ubalozi huo.
Mashambulizi ya Israel mjini Doha yalikuwa ya kwanza aina yake katika mji mkuu wa Qatar, ambako Hamas ilisema ujumbe wake ulikuwa ukikutana kujadili mpango wa usitishaji mapigano wa Gaza unaoungwa mkono na Marekani.
Kundi la Hamas la Palestina limesema mashambulizi hayo yaliwaua watu sita, wakiwemo mtoto wa mpatanishi wake mkuu na afisa wa usalama wa Qatar, lakini viongozi wakuu wa kundi hilo walinusurika.
Qatar, pamoja na Marekani na Misri, imekuwa ikicheza jukumu muhimu katika jitihada za kusitisha vita vya Israel dhidi ya Gaza, ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 64,000 tangu Oktoba 2023.