Katika Mkutano wa Pili wa kujadili Mabadiliko ya tabia nchi unaoendele nchini Ethiopia, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed alitangaza kwa fahari ombi la Ethiopia kuwa mwenyeji wa COP 32 mnamo 2027, na kuualika ulimwengu kushuhudia uongozi wa Afrika katika suluhisho la hali ya hewa.
Mkutano wa Wanachama (COP) ndio chombo kikuu cha maamuzi cha Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).
Waziri Mkuu Abiy aliwasilisha ‘Mpango wa Urithi wa Kijani wa Ethiopia’ kama mfano mkuu wa kujitolea kwa nchi hiyo katika kukabiliana na hali ya hewa.
"Mnamo mwaka wa 2019, tulizindua mpango wa ‘Green Legacy.’ Katika miaka saba, tumepanda zaidi ya miche bilioni 48. Inapoza ardhi yetu, inarutubisha udongo wetu, inarejesha vyanzo vya maji, hutoa chakula, kuunda nafasi za kazi, na kuongeza mauzo ya nje," aliuambia mkutano huo unaofanyika Addis Ababa.
Waziri Mkuu alibainisha kuwa "upandaji miti si mradi wa majaribio, bali ni utamaduni," akisisitiza kuwa hii ni juhudi endelevu, inayoendeshwa na jamii badala ya mpango wa muda.
Kila mwaka, wawakilishi kutoka nchi zote ambazo ni "Washiriki" katika Mkataba wa Paris hukusanyika ili kukagua maendeleo kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, kujadili makubaliano mapya, na kuweka malengo ya siku zijazo.
Nchi zilizowahi kuwa wenyeji wa COP Afrika
Kenya ilikuwa mwenyeji wa mkutano huu wa kimataifa mwaka 2006 jijini Naiorbi, Morocco ilikuwa mwenyeji 2001 na 2016.
Afrika Kusini ililkuwa mwenyeji 2011 na Misri 2022.
Mikutano ya COP ni jukwaa muhimu kwa sera ya hali ya hewa duniani, inayoleta pamoja serikali, wanasayansi, na jumuiya za kiraia kushughulikia suala kubwa la mabadiliko ya hali ya hewa.
Kuandaa mkutano wa COP ni kazi muhimu inayohitaji taifa kuonyesha sifa dhabiti za hali ya hewa na uwezo wa kuhudumia maelfu ya wajumbe.
Nchi mwenyeji wa mikutano ya COP kawaida huzunguka kati ya makundi matano ya kikanda ya Umoja wa Mataifa: Afrika, Asia-Pacific, Ulaya Mashariki, Amerika ya Kusini na Karibiani, na Ulaya Magharibi na nyingine.
Ili kuamua ni nchi gani itaandaa mkutano huo wa kimataifa, washiriki wa kikundi cha kikanda wanajadili na kuchagua nchi ya itakayowasilisha rasmi ombi kwa UN.
Nchi inapochaguliwa, hutuma ombi rasmi la kuandaa mkutano huo.
Timu ya Umoja wa Mataifa hutembelea ili kuhakikisha nchi inaweza kushughulikia vifaa, mahitaji ya kifedha, na mahitaji ya kiufundi.
Baada ya kuidhinishwa, nchi mwenyeji hutoa mahali, vifaa, na huduma, ikiwa ni pamoja na tafsiri katika lugha sita za Umoja wa Mataifa, ili kuhakikisha mawasiliano mazuri wakati wa tukio.
"Tunaialika dunia katika mji mkuu wa Afrika wa diplomasia na matarajio ya hali ya hewa - kushuhudia suluhisho letu na kusaidia kuunda mkutano huo kwa siku zijazo. Hebu tuonyeshe ulimwengu kwamba bara la asili pia litakuwa bara la suluhisho," Waziri Mkuu alisema.