Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC inaendelea kusikiliza kesi dhidi ya Joseph Kony, raia wa Uganda aliyeongoza kikundi cha uasi nchini Uganda.
Kony alidai kuwa alitaka kuongoza Uganda kupitia amri kumi za Mungu.
Kulingana na Umoja wa Mataifa shughuli za LRA ziliua takriban watu 100,000 na kuwalazimisha takriban milioni 2.5 barani Afrika kuhama makwao kati ya 1986 na 2009.
ICC iliamuru akamatwe 2005 lakini hadi sasa wakati kesi yake inaanza kusikilizwa bila ya yeye mwenyewe kuwepo.
Kundi la LRA lilifurushwa kutoka Uganda mwaka 2005, na waasi hao wakaingia katika lililokuwa eneo la Sudan na hatimaye kuweka kambi katika mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Baadaye walihamia Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako inafahamika walijihusisha na ujangili na uchimbaji madini haramu.
Kulikuwa na majaribio ya serikali ya Uganda kufanya makubaliano ya amani na Kony, lakini mazungumzo yalivurugika mwaka 2008 kwa sababu kiongozi huyo wa LRA alitaka kuhakikishiwa usalama wake na washirika wake.
Na sasa kesi yake iko mbele ya mahakama, huku akiwakilishwa na wakili aliyeteuliwa na mahakama.
ICC inadai kumshtaki kwa makosa 39 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, yakiwemo mauaji, ubakaji, kutumia watoto kama wanajeshi, na utumwa wa jinsia, kati ya 2002 na 2005.
Kamanda mwengine wa LRA, Dominic Ongwen, alihukumiwa na ICC mwaka 2020 kwa makosa 61 yanayofanana na yale ya Kony.
Ongwen mwenyewe alitekwa nyara na wanamgambo akiwa kijana wa miaka 9, akabadilishwa na kuwa mwanajeshi mtoto na baadaye kuwa kamanda katika kundi hilo la waasi.
Kwa sasa Ongwen anatumikia kifungo chake cha miaka 25 nchini Norway.
Wakati kesi ya Joseph Kony inaposikilizwa waathirika bado wanasubiri kwa hamu kuona hukumu itakayotolewa.
Lakini raia wengine wa Uganda wanadai kuwa kuanza kesi ya Kony bila yeye mwenyewe kuwepo au bila kujua hata kama ako hai haina uzitoi kwani hata akipatikana kuwa na hatia haki haitatendeka ikiwa hatakamatwa.