ULIMWENGU
2 dk kusoma
UN imepitisha Azimio la New York la kuundwa kwa taifa la Palestina
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) limepitisha azimio lililopendekezwa na Ufaransa na Saudi Arabia linalounga mkono kuundwa kwa taifa la Palestina na suluhisho la mataifa mawili; nchi 142 zimepiga kura ya kuunga mkono.
UN imepitisha Azimio la New York la kuundwa kwa taifa la Palestina
Riyad H Mansour, Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, akiwa kwenye skrini akiwahutubia wajumbe baada ya kura ya UNGA. / / Reuters
tokea masaa 8

Siku ya Ijumaa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha na kuunga mkono Azimio la New York, ambalo linakusudia kutambua taifa la Palestina na kushinikiza juhudi za kufanikisha suluhisho la mataifa mawili katika mzozo wa Israel na Palestina.

Azimio hilo, ambalo kwa jina rasmi linaitwa: “Kuunga Mkono Azimio la New York kuhusu Utatuzi wa Amani wa Swala la Palestina na Utekelezaji wa Suluhisho la Mataifa Mawili,” lilipitishwa kwa kura 142, hata hivyo nchi10 zimepinga azimio hilo, huku nchi 12 zimesusia kupiga kura.

Azimio hilo liliwasilishwa na Ufaransa na Saudi Arabia, na tayari lilikuwa limesainiwa na nchi wanachama 17 wakati wa mkutano wa kimataifa uliofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York mnamo Julai.

Jerome Bonnafont, Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, alisema:

“Azimio hili ni matokeo ya kazi iliyofanyika wakati wa mkutano kati ya tarehe 28 hadi 30 Julai, 2025 huko New York, na liliandikwa kwa ushirikiano na wenyeviti wenza 17. Azimio hili linaweka ramani ya pamoja ya njia ya kufanikisha suluhisho la mataifa mawili.”

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, aliwashukuru mataifa yote yaliyoliunga mkono azimio hilo, na kusema: “Kwa wale wanaotaka amani, njoni muungane nasi. Kwa wale wanaotaka kuokoa maisha, njoni muungane nasi.”

Hata hivyo, Israel na Marekani walipinga azimio hilo.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon, alisema:

“Kuunga mkono azimio hili linaloitwa la amani si juhudi ya kweli ya kuleta amani.”

Mwakilishi wa Marekani, Morgan Ortagus, naye aliongeza kuwa: “Maandishi haya yanadhoofisha juhudi za kweli za kidiplomasia kumaliza mgogoro huu,” akisema pia kuwa “yamewatia nguvu Hamas na kudhuru matumaini ya kufikia amani.”

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us