Vijana wanaotumia sigara mvuke wako katika hatari na uwezekano mkubwa wa kuanza kuvuta sigara za kawaida na pia hukabiliwa na hatari kubwa zaidi za kiafya, kulingana na utafiti uliofanywa na vyuo vikuu vya York na London School of Hygiene and Tropical Medicine (LSHTM).
Utafiti huo, maarufu kama “rejeo la marejeo,” ulibaini ushahidi wa mara kwa mara wenye kuonesha uhusiano kati ya matumizi ya sigara mvuke na uvutaji wa sigara za kawaida hapo baadaye.
Pia ulihusisha matumizi ya sigara hizo na maatizo ya kiafya kama vile pumu, kukohoa, muwasho wa njia ya hewa, matatizo ya afya ya akili, na matumizi ya dawa nyingine za kulevya.
Watafiti walisisitiza umuhimu wa utafiti zaidi ili kuthibitisha uhusiano wa sababu na athari, lakini pia waliongeza kuwa ushahidi uliopo unatosha kuunga mkono sera za tahadhari, ikiwemo kudhibiti zaidi upatikanaji wa sigara za mvuke kwa vijana na kuimarisha kampeni za elimu ya umma.
Matumizi ya mara kwa mara ya sigara mvuke yanaongeza hatari
Dkt. Su Golder, Profesa Mshiriki wa Sayansi ya Afya kutoka Chuo Kikuu cha York, alisema kuwa tafiti za awali tayari zilionyesha kuwa matangazo ya sigara za mvuke kwenye mitandao ya kijamii yanachangia vijana kuanza kuvuta.
Katika uchambuzi wa sasa, alisema, hali inazidi kuwa ya kutia wasiwasi hasa pale matumizi haya yanapokuwa ya mara kwa mara.
“Uthibitisho uliopatikana ni wa kushangaza,” alisema Dkt. Golder. “Katika tafiti mbalimbali, vijana wanaotumia sigara za mvuke wana uwezekano mkubwa wa kuanza kuvuta sigara.”
“Matokeo haya yanaunga mkono hatua madhubuti za afya ya umma kulinda vijana dhidi ya madhara ya matumizi ya sigara za kielektroniki,” aliongeza.
Uchambuzi ulionyesha kuwa vijana wanaoanza kuvuta sigara za mvuke huwa na uwezekano mkubwa wa kuhamia kwenye sigara za kawaida, na pia wanaweza kuvuta mara kwa mara au kwa wingi zaidi.
Aidha, matumizi ya sigara za mvuke yalihusishwa na kuanza kutumia pombe na bangi kwa baadhi ya vijana.
Matatizo ya afya ya akili
Utafiti huu ulionyesha pia uhusiano kati ya matumizi ya sigara za mvuke na matatizo ya mfumo wa upumuaji kama vile pumu na muwasho kwenye sehemu ya kupita hewa.
Pia kulikuwa na uhusiano wa kutia wasiwasi kati ya matumizi hayo na msongo wa mawazo au mawazo ya kujiua kwa vijana, ingawa wataalamu walionya kuwa utafiti zaidi unahitajika kuelewa kwa kina madhara ya kiafya ya akili.
Vijana wengi waliripoti utegemezi wa nikotini, ikiwa ni pamoja na hamu ya mara kwa mara na ugumu wa kuacha kutumia. Hata hivyo, licha ya wasiwasi kuhusu athari za nikotini kwenye ubongo wa kijana unaoendelea kukua, tafiti chache zimechunguza suala hilo kwa undani.
Dkt. Greg Hartwell, Profesa Msaidizi wa Kliniki katika LSHTM, alisema:
“Uchambuzi wetu unatoa picha pana zaidi hadi sasa kuhusu aina mbalimbali za madhara ya matumizi ya sigara za kielektroniki kwa vijana.”
“Kwa namna ya kipekee, tumegundua ushahidi wa mara kwa mara unaoonyesha kuwa matumizi haya hupelekea kuvuta sigara, jambo ambalo linafungua mlango kwa madhara mengi ya kiafya yatokanayo na sigara za kawaida,” aliongeza.
Wito wa utafiti wa haraka na marufuku ya uuzaji
Watafiti walihimiza kufanyika kwa tafiti za kuendelea kuhusu jinsi sigara za mvuke zinavyoathiri ukuaji wa ubongo, afya ya moyo na mishipa, afya ya mdomo, pamoja na madhara ya kutumia kwa pamoja tumbaku na sigara za mvuke.
Walisema kuwa hadi mapungufu haya ya utafiti yatakapozibwa, ni muhimu kwa mamlaka za afya kuchukua hatua za tahadhari ili kuwalinda vijana dhidi ya madhara ya muda mrefu.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2023, jumla ya nchi na maeneo 121 tayari yameweka kanuni kuhusu matumizi ya vifaa vya kielektroniki vya kusambaza nikotini.
Kati ya hizo, 33 zimepiga marufuku kabisa uuzaji, huku 87 zikiwa zimeweka hatua kama vile umri utakaoruhusiwa kutumia sigara hiyo , marufuku ya matangazo, na kupiga marufuku matumizi katika maeneo ya umma ya ndani.
Hata hivyo, bado kuna ukosefu wa usawa katika udhibiti.
Ripoti hiyo ilibaini kuwa nchi 74 — zenye jumla ya watu zaidi ya bilioni mbili — hazina sheria yoyote kuhusu sigara za mvuke.
Hii inajumuisha asilimia 40 ya nchi za kipato cha kati na karibu asilimia 80 ya zile za kipato cha chini, ambazo bado hazijachukua hatua za kisheria kudhibiti bidhaa hizi.