Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) umeshtumu “vikali” mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Allied Democratic Forces (ADF) ambayo yaliwaua raia wasiopungua 52 mashariki mwa nchi.
ADF ililenga maeneo ya Beni na Lubero katika mkoa wa mashariki wa Kivu Kaskazini kuanzia Agosti 9 - 16 ikiwemo mauaji ya wanawake wanane na watoto wawili, taarifa ya MONUSCO ilisema siku ya Jumatatu.
Bintou Keita, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Congo na kiongozi wa MONUSCO, anasema mashambulizi, yanakuja baada ya mashambulizi ya ADF katika kanisa moja mwishoni mwa mwezi Julai, ambayo yalikuwa “ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za binaadamu za kimataifa,.”
Mashambulizi ya eneo la Komanda katika mkoa wa Ituri yaliwaua raia 43.
Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umeomba Mamlaka ya Congo kuchunguza ukatili huo na kuwawajibisha wale wote waliohusika.
MONUSCO inasema imeimarisha uwepo wake Kivu Kaskazini na Ituri kupitia doria, kupeleka vikosi na kufanya uratibu na mamlaka za maeneo mbali mbali ili kuwalinda raia na kuhakikisha amani katika maeneo yaliyoathirika.