Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan na mwenzake wa Marekani Marco Rubio wamejadili matokeo ya mkutano wa Washington kati ya Rais wa Marekani Trump na Rais wa Ukraine Zelenskyy na viongozi wengine wa Ulaya
Katika mazungumzo kwa njia ya simu siku ya Jumanne, pia walijadili matokeo ya mkutano kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin Alaska Agosti15, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki.
Walizungumzia kuhusu hatua zitakazochukuliwa kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine, huku Fidan akieleza utayari wake wa kutoa usaidizi wowote unaohitajika kwa lengo la kupata amani ya kudumu na ya haki.
Maafisa hao wawili walikubaliana kuhusu haja ya kumaliza mauaji kati ya mataifa hayo mawili yanayopigana, kulingana na taarifa kutoka kwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Tommy Pigott.
Kuendelea kuunga amani Ukraine
Makamu wa Rais wa Uturuku Cevdet Yilmaz alisema Jumanne kuwa Uturuki itaendelea kuunga mkono juhudi za kidiplomasia zinazolenga kupata "amani ya haki na ya kudumu" Ukraine.
"Tutaendelea kuunga mkono kikamilifu juhudi za kidiplomasia kwa amani ya haki na ya kudumu," Yilmaz alisema katika mtandao wa kijamii wa Uturuki NSosyal.
Yilmaz pia alishiriki katika mkutano kwa njia ya video wa Jumanne na kundi la "washirika wa nia njema" kwa niaba ya Rais Recep Tayyip Erdogan, kufuatia mikutano ya awali iliyofanyika Agosti 13 na 17.
"Katika mkutano huo kwa njia ya video, washiriki walibadilishana mawazo na kufanya tathmini kuhusu mazungumzo ya Alaska kati ya marais wa Marekani na Urusi, pamoja na majadiliano ya jijini Washington kati ya Rais Trump, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, viongozi kadhaa wa nchi za Ulaya, na wawakilishi wa EU na NATO," Yilmaz alieleza.
Alieleza kuwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande zote hivi karibuni yanaweza kuwa "hatua mpya" ya diplomasia. Hatua hiyo, inayoongozwa na Uingereza na Ufaransa, inapanga kupeleka vikosi vya kulinda amani kutoka mataifa kadhaa ya Ulaya na NATO baada ya kumalizika kwa vita vya Ukraine.
Siku ya Jumatatu Trump alisema viongozi walijadili hakikisho la usalama kwa Ukraine, na serikali yake kuanza maandalizi ya mkutano kati ya Putin na Zelenskyy, na baadaye mkutano wa utatu utakamjumuisha yeye.
Mkutano wa Washington unakuja baada ya mkutano wa Trump na Putin katika jimbo la Marekani la Alaska wenye lengo la kumaliza vita nchini Ukraine.