Afrika
4 dk kusoma
Ramadhan 2025: Zaidi ya kufunga-Mwezi wa rehema na maana
Ramadhan ni wakati wa kuimarisha imani na mazingatio makubwa kwa binadamu, ambayo yanatoa njia ya mabadiliko ya ndani ya jamii.
Ramadhan 2025: Zaidi ya kufunga-Mwezi wa rehema na maana
Ibada ya saum ya Ramadhan
4 Machi 2025

Ramadhan, mwezi mtukufu na wenye umuhimu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, umewadia. Wikendi hii, karibu Waislamu bilioni mbili duniani kote wataanza funga yao mwezi mzima. Wakati huu, wao hufunga kutoka alfajiri hadi kutua kwa jua, wakiacha kula na kunywa katika muda huu wote. Iwapo huifahamu Ramadhan, hapa kuna mambo machache muhimu ya kujua.

Ramadhan ni wakati wa kuimarisha upya imani, kukuza nidhamu, kutoa shukrani, na kuunganisha watu zaidi - matokeo yake ni zaidi ya kutokula na kunywa nyakati za mchana.

Wakati manufaa ya afya ya kimwili ya funga yamekuwepo kwa muda mrefu, pamoja na hizo, kuna njia nyingi ambazo Ramadhan pia huimarisha katika imani ya mwanadamu. Vipengele vichache vinajitokeza hasa.

Kufunga kwa ajili ya nafsi

Mtume Muhammad (SAW) aliwahimiza waumini kufuata utaratibu wa mfungo wa kiimani kwa kuondoa vikengeusha-fikira—kama vile kula na kunywa—na kuzingatia uhusiano wa ndani zaidi na Mungu.

Ramadhan inakuwa wakati wa kutafakari kwa kina kiimani na kuwa na mazingatio, kuwapa wale wanaoitekeleza fursa ya kutulia, kurekebisha, na kujitahidi kuelekea katika kuwa hali o bora. Kimsingi, mabadiliko haya yanatakiwa kuwa zaidi ya mwezi, yakijenga tabia na matendo yao mwaka mzima.

Kama mwanachuoni wa Kiislamu wa mwanzoni mwa karne ya 20 Bediüzzaman Said Nursi alivyoeleza, lengo ni kuimarisha ndani na nje ya moyo wako wakati wa mfungo na kujisogeza karibu zaidi kiimani kama ilivyoamrishwa na taratibu za dini ya Kiislamu.

Kujiweka mbali na hisia na vitendo hasi visivyofaa ni moja ya matamanio katika funga. Zaidi ya hapo awali, Waislamu hujaribu kujiepusha na vitendo vibaya kama kusengenya, hasira na ukosefu wa uaminifu. Mtazamo ni juu ya kujitakasa binafsi na kuendeleza maadili mema.

Katika mchakato huu wa ibada kamili na tafakuri ya kina, mfungaji huweka juhudi za kukuza umakini zaidi na fadhila zingine muhimu kama huruma, upole, unyenyekevu, subira, uvumilivu na ustahimilivu. Hapa, Qur’an - iliyoteremshwa kwa mara ya kwanza katika mwezi wa Ramadhan - ndio mwongozo wa mwisho wa kupitia msimu huu wa mabadiliko ya kiimani.

Ramadhan hukumbusha watu kujizuia kwa upole na wastani, kwamba kurudi kwa mambo muhimu ni afya ya mwanadamu.

Kula kwa vipimo

Kula vyakula vingi vya kusindika na utumiaji kupita kiasi sio faida kwa maisha ya afya. Maisha ya urahisi na kuridhika huruhusu mtu kuwa na afya njema. Inahifadhi vyema maliasili za dunia hii.

Ubadhirifu unatakiwa kuepukwa. Kuelewa kwamba mtu hahitaji mengi ili kuridhika ni ni jambo la msingi sana kipindi hiki. Wakati huo huo, Ramadhan huongeza shukrani na kuthamini vitu vilivyopo kama vile maji na chakula.

Umuhimu pia unajumuisha kupunguza usumbufu, kuuondoa moyo kutoka kwa mzigo wote mzito na kujiweka huru na jambo lolote la madhila. Kujitenga na mafadhaiko na wivu na kuzuia maisha ya kupenda vitu vya kimwili ni njia nzuri za kuleta mazingatio.

Kuimarisha mahusiano

Chakula ambacho mtu hufurahia mwisho wa siku mara nyingi huandaliwa na watu kwa pamoja. Zaidi ya hapo awali, Ramadhan hutumika kama ukumbusho wa kutegemeana kwa wanadamu na hitaji letu la kimsingi la kujumuika.

Watu hujumuika na kuimarisha mshikamano na upendo. Hakika Ramadhan inawaleta pamoja watu kushirikiana katika chakula na kuimarisha ukaribu na ukarimu wa watu katika jamii.

Katika wakati huu wa utoaji, Waislamu kwa kawaida hutoa asilimia 2.5 ya mali zao kwa wahitaji kama utimilifu wa sadaka yao ya lazima (zakat).

Pia baadhi yao wanafanya shughuli za hisani kama kuwa na iftari kadhaa za jamii na kuwaalika majirani zao wasio Waislamu kujiunga nao katika milo hiyo. Hafla hizi ni fursa nzuri ya kujifunza na watu kuungana.

Kwa kuongezea, kukuza uhusiano mzuri wa kijamii na wa maana ni ufunguo wa kustawi kwa mwanadamu.

Mwezi mtukufu huwa ni fursa kwa watu kukuza mahusiano ya kijamii. Upweke ni hatari kwa afya ya binadamu. Kwa wanaofunga huwa ni nafasi ya kuleta nguvu kwa jamii na ustawi kwa jumla.

Kufunga pamoja, kutumia muda mwingi katika maombi ya jumuiya, kuzingatia matendo ya fadhila na misaada - yote haya husaidia kukabiliana na kutengwa na kukuza hisia zaidi ya kuhusishwa.

Kutunza familia, jamaa, marafiki, majirani na wanadamu wenzetu ni kanuni muhimu ya mfungo wa jumla.

Kufanya jitihada za kuacha kinyongo na chuki, kujaribu kusameheana na kupatanisha ni njia zote za kutakasa moyo kutokana na uzito wote usio wa lazima.

Kwa sababu zote hizi na nyingi zaidi, Ramadhan imeelezwa kuwa njia ifaayo kuwa ni mwezi wa rehema na mara zote Waislamu huwa na mtazamo wa kuimarishwa upya kiimani. Kwa kuzingatia kujiendeleza kwa mtu binafsi na kujenga jamii iliyo imara, wasio Waislamu pia wanaweza kupata faida nyingi ya msimu huu wa kiimaniwa Ramadhan.

Mwandishi, Zeyneb Sayilgan, PhD, ni mwanazuoni wa Kiislamu katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislamu aliyebobea katika teolojia ya Kiislamu, uhusiano wa Wakristo na Waislamu, na makutano ya dini na uhamiaji.


Maoni yaliyotolewa na mwandishi si lazima yaakisi maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.


Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us