AFRIKA
2 dk kusoma
Sudan inakaribisha juhudi za amani kumaliza vita na RSF, inakataa kuingiliwa na mataifa ya kigeni
Matamshi ya Sudan yanakuja baada ya taarifa ya pamoja ya Misri, Saudi Arabia, Imarati na Marekani kutaka kufikiwe makubaliano ya kibinadamu ili kuruhusu misaada katika maeneo yote ya Sudan.
Sudan inakaribisha juhudi za amani kumaliza vita na RSF, inakataa kuingiliwa na mataifa ya kigeni
Kikosi cha RSF na jeshi wamekuwa katika vita kali vya kupigania madaraka tangu Aprili 2023, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu. / Reuters
tokea masaa 12

Sudan imekaribisha juhudi zinazolenga kumaliza vita nchini humo na mashambulizi yanayofanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), huku ikisisitiza kukataa kuingiliwa kwa masuala ya ndani na mataifa ya kigeni.

"Serikali ya Sudan inakaribisha juhudi zozote za kikanda au kimataifa za kusaidia kumaliza vita, kusitisha mashambulizi ya kigaidi ya wanamgambo wa RSF kwenye miji na miundombinu, na kuondoa mzingiro kwenye miji ili kuhakikisha kwamba maafa na uhalifu dhidi ya watu wa Sudan hayarudiwi tena," ilisema Wizara ya Mambo ya Nje katika taarifa iliyotolewa kwenye X siku ya Jumamosi.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya tamko la pamoja kutoka Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Marekani likitoa wito wa "sitisho la kibinadamu" nchini Sudan ili kuruhusu misaada kuingia haraka katika sehemu zote za nchi.

Mapigano El-Fasher

Wizara hiyo ilirudia msimamo wake wa kukataa "kuingiliwa kwa kimataifa au kikanda ambako hakuheshimu mamlaka ya Sudan, taasisi zake halali, na haki yake ya kulinda watu wake na ardhi yake."

Ilielezea masikitiko yake kuhusu kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kulazimisha RSF "kutekeleza Maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2736 na 1591, kuondoa mzingiro kwenye mji wa El-Fasher, kupunguza mateso ya raia wake, wakiwemo wazee, wanawake, na watoto, na kuruhusu kupita kwa misafara ya misaada."

El-Fasher imekuwa ikishuhudia mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na RSF tangu Mei 2024, licha ya onyo la kimataifa kuhusu hatari ya ghasia katika mji huo ambao ni kitovu muhimu cha kibinadamu kwa majimbo matano ya Darfur.

RSF na jeshi wamekuwa wakihusika katika mvutano mkali wa madaraka tangu Aprili 2023, hali ambayo imesababisha maelfu ya vifo na kuisukuma Sudan katika moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Zaidi ya watu 20,000 wameuawa na wengine milioni 15 kuyahama makazi yao, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa na vyanzo vya ndani.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us