Makamu wa Rais wa Uturuki amesema kuwa nchi yake imesisitiza kuwa tayari kuchukua uongozi katika nyanja zote kuhakikisha amani ya kudumu katika vita kati ya Urusi na Ukraine.
Katika ujumbe aliotoa kwenye mtandao wa kijamii wa Uturuki, NSosyal, Cevdet Yilmaz alisema Alhamisi kwamba alihudhuria mkutano wa tano wa Viongozi wa Muungano Unaounga Mkono Ukraine kwa njia ya mtandao, ambapo alikuwa amehudhuria mara nne awali akimwakilisha Rais Recep Tayyip Erdogan.
“Katika kikao hicho, kilichoandaliwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, jitihada za kidiplomasia za kufanikisha amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine kufuatia hatua iliyochukuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump zilijadiliwa,” alisema Yilmaz.
“Uturuki inasisitiza tena kuwa tuko tayari kuchukua jukumu la uongozi katika nyanja zote kuhakikisha amani ya kudumu, na kwamba diplomasia na mazungumzo kati ya pande zote zinazohusika inatakiwa kupewa kipaumbele. Hadi amani ya haki na ya kudumu itakapopatikana, tutaendelea kuchangia katika mchakato wa kidiplomasia kwa kutumia kila njia tulizo nazo,” aliongeza.
Kauli hiyo ilitolewa baada ya mkutano wa Alaska uliofanyika mwezi uliopita kati ya Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin, ambapo jitihada za kufikia usitishaji wa mapigano pamoja na kupanga mkutano kati ya Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy zinaendelea kwa kasi.
Uturuki, kama nchi rafiki ya Urusi na Ukraine, imechukua nafasi ya kipekee na ya moja kwa moja katika jitihada za kumaliza vita vilivyoanza Februari 2022.