Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesisitiza kuwa Uturuki haitakaa kimya wakati Wapalestina wakiteseka chini ya mashambulizi ya Israel, akimsuta Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
"Hatuwezi kukaa kimya kama watazamaji wa mateso huko Palestina au ukandamizaji wa dhalimu, yule kafiri anayeitwa Netanyahu," Erdogan alisema Jumatano, akihutubia tukio la ufunguzi wa Wiki ya ‘Mevlid-i Nebi’ ambayo ni hafla ya kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), iliofanyika jijini Ankara.
Rais aliongeza kuwa wasiwasi wa Uturuki unaenea nje ya mipaka yake, akisisitiza mshikamano na mataifa ya Kiislamu yaliyokumbwa na migogoro.
"Nusu ya mioyo yetu iko hapa; nusu nyingine iko Gaza, Palestina, Yemen, Sudan na Afghanistan, ambapo majeraha ya ulimwengu wa Kiislamu yanavuja damu," alisema.
Akisisitiza mada ya umoja, Erdogan alisema: “Tunaona Waislamu wote kama matofali ya jengo moja, na viungo vya mwili mmoja.”
Licha ya machafuko katika eneo lote, rais alihimiza kuwe na uvumilivu na ukaidi.
"Sisi sio watu wasio na matumaini, na hatutakosa matumaini kamwe. Licha ya dhuluma, ukosefu wa usawa na uonevu katika jiografia yetu, hatutaweza kukata tamaa," alisema.
Israel ilifanya mashambulizi ya kikatili ya kijeshi huko Gaza, na kuua zaidi ya Wapalestina 63,700 huko Gaza tangu mwishoni mwa 2023.
Mashambulizi ya kijeshi yameharibu eneo hilo, ambalo linakabiliwa na njaa iliyosababishwa na Israel.
Tarehe 8 Agosti, Baraza la Mawaziri la Usalama la Israel pia liliidhinisha mpango wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa kuikalia Gaza hatua kwa hatua, kuanzia mji wa Gaza.
Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.
Israel pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa vita vyake dhidi ya eneo hilo.