Watu wasiopungua 20 wameuawa katika mji wa Mathiang, jimbo la Upper Nile lililopo kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, baada ya mapigano makali kuibuka kati ya vikosi vya serikali, wapiganaji wa upinzani, na makundi yenye silaha, vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti siku ya Jumanne, vikitaja vyanzo vya kijeshi.
Mapigano yalizuka mapema Jumatatu huko Mathiang wakati wapiganaji wa Sudan People’s Liberation Movement-in-Opposition (SPLA-IO) na wale wa White Army waliposhambulia maeneo ya wanajeshi wa Sudan Kusini (SSPDF), afisa mmoja mwandamizi wa jeshi amekiambia kituo cha redio cha Tamazuj siku ya Jumanne.
Mapigano yaliendelea kwa karibu saa tatu na kusababisha mauaji ya wanajeshi wanne wa SSPDF na wapiganaji 16 wa SPLA-IO, Meja Jenerali Khor Chuol Giet alikiambia kituo hicho.
“Tumekuta miili yao 16 katika mahandaki, lakini huenda kukawa na miili zaidi,” aliongeza.
Hali tete
Sudan Kusini, ilipata uhuru wake kutoka kwa Sudan 2011 kufuatia kura ya maoni.
Hata hivyo, imekuwa kwenye mapigano tangu Disemba 2013, wakati Rais Salva Kiir Mayardit alipomfuta kazi na kumshtumu Makamu wa Rais wakati huo Riek Machar kwa kupanga njama ya kumpindua.
Licha ya kuwepo kwa makubaliano ya amani ya 2018 na 2022, bado hali imekuwa tete.
Mwezi FebruarI, kundi la wapiganaji linalojulikana kama White Army, ambalo linamuunga mkono Machar, lilichukuwa udhibiti wa mji mmoja katika Jimbo la Upper Nile. Kufuatia hatua hiyo, majenerali kadhaa na mawaziri wa serikali walio upande wa SPLA-IO ya Machar walikamatwa.