AFRIKA
2 dk kusoma
DR Congo yashtumu waasi wa M23 kwa kukiuka haki za binadamu, kulazimisha watu kujiunga nao
Utekaji nyara wa vijana unaendelea, hadi kulazimisha watu kujiunga nao katika mapigano , amesema afisa mmoja
DR Congo yashtumu waasi wa M23 kwa kukiuka haki za binadamu, kulazimisha watu kujiunga nao
tokea masaa 19

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Jumanne imeshtumu waasi wa M23 kwa kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu na kulazimisha vijana kujiunga na mapigano ya uasi mashariki mwa nchi.

Akihutubia waandishi wa habari katika mji mkuu Kinshasa kuhusu hali ya usalama ya nchi hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani Jacquemain Shabani anasema serikali imegundua kuwa waasi wamekiuka haki za binadamu dhidi ya raia katika maeneo yaliyokaliwa mashariki mwa Congo ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini.

“Hali ya usalama ni ile ile hasa kwa upande wa ukiukwaji wa haki za binadamu. Tunaendelea kila siku kurekodi ukiukwaji wa haki za raia wetu wenyewe ambao wanaishi katika mazingira magumu, kutokana na ukosefu wa usalama,” alisema.

“Lazima ieleweke kuwa utekaji nyara wa vijana unaendelea, na kuwapeleka kwa lazima katika kujiunga nao kwenye mapigano.”

Mashariki mwa Congo kumekumbwa na machafuko kwa miongo kadhaa.

Kurejea tena kwa waasi wa M23 mwaka 2021, wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, kumetatiza hali ya mapigano zaidi.

Kundi hili linadhibiti eneo kubwa, ikiwemo makao makuu ya mikoa, Goma na Bukavu, ambayo walidhibiti mapema mwaka huu.

Mwezi Julai, Congo na makundi mengine ya waasi ikiwemo M23 (AFC/M23) walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano Doha yaliyojulikana kama Azimio la Kimsingi.

Lakini vita mashariki mwa Congo vinaendelea huku wakishtumiana kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Shabani alikiri kuwa kumekuwepo kwa ukiukwaji wa kusitishwa mapigano huku mazungumzo yakiendelea huko Doha “kwa bahati mbaya bado ni changamoto kubwa” pamoja na kuanzishwa kwa serikali sanjari na waasi.

M23 imekuwa ikikanusha taarifa za awali za kukiuka haki za binadamu.

Lakini mwezi uliopita, shirika la Amnesty International lilishtumu makundi yanayozozana ikiwemo waasi wa M23 na Wazalendo, wapiganaji wanaoungwa mkono na serikali huko mashariki mwa Congo, kwa kuhusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo ubakaji, mauaji ya kiholela na utekaji nyara.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us