Waziri wa mambo ya nje wa Misri ametoa wito wa kufanyika mabadiliko makubwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisema muundo wake wa sasa hauakisi uhalisia wa enzi hizi na halitendei haki bara la Afrika, nchi za Kiarabu, na zile za Kiislamu.
Akizungumza katika Jukwaa la Kimkakati la Bled huko Slovenia, Badr Abdelatty amesema kuwa uhusiano wa mataifa mengi hauwezi kufikiwa bila kufanya mabadiliko ya kitaasisi.
“Baraza la Usalama na taasisi za Bretton Woods (Benki ya Dunia na IMF) lazima zifanyiwe mabadiliko. Bila haya, mazungumzo ya uongozi wa dunia na uhusiano wa mataifa hayana maana,” aliliambia jopo kuhusu mchakato huo siku ya Jumanne.
Mjadala kuhusu kura ya turufu
Amesema si sahihi kuwa bara zima la Afrika halijawakilishwa kwa nafasi ya kudumu katika Baraza la Usalama.
“Kuwapa uwezo wa kura ya turufu nchi tano pekee ni suala lililopitwa na wakati na lisilo la kidemokrasia,” Abdelatty alisema, akiongeza kuwa haki hiyo iongezwe kwa wanachama wapya au iondolewe moja kwa moja.
Abdelatty alishtumu serikali za magharibi kwa undumakuwili, akieleza tofauti ya namna masuala ya uvamizi wa Ukraine na Urusi na vita vya Israel huko Gaza yalivyoshughulikiwa.
“Katika mataifa ya Magharibi, mara kwa mara naskia wanazungumzia kuhusu kukaliwa,” alisema. “Lakini inapokuja suala la Gaza na kanda yetu, tatizo hilo hilo haliangaziwi. Hii ni aibu kwa mataifa ya Magharibi na ubinadamu.”
Msimamo dhidi ya Israel
Alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwa na msimamo dhidi ya mauaji ya halaiki ya Israel yanayoendelea huko Gaza na kutekeleza sheria ya kimataifa bila upendeleo, wala kuegemea upande.
Israel imewaua Wapalestina zaidi ya 63,600 Gaza tangu Oktoba 2023. Jeshi limeharibu kabisa Gaza, ambayo inakabiliwa na njaa kali.
Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa (ICC) ilitoa vibali vya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu Gaza.
Israel pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa vita vyake huko Gaza.