UTURUKI
3 dk kusoma
Uturuki kuzidi uwezo wa meli ya kivita ya Ufaransa 'Charles de Gaulle' - ripoti
Uturuki inatarajiwa kujiunga na kundi dogo la mataifa yenye uwezo wa kujenga meli kubwa za kubebea ndege zenye usanifu wa hali ya juu wa kivita, kwa mujibu wa ripoti kutoka Ufaransa.
Uturuki kuzidi uwezo wa meli ya kivita ya Ufaransa 'Charles de Gaulle' - ripoti
Uturuki tayari imepiga hatua katika kuimarisha ulinzi wa majini kwa kutumia chombo cha kwanza duniani cha kubeba ndege za kivita zisizo na rubani. / / AA
3 Septemba 2025

Gazeti la Le Figaro la Ufaransa limeripoti kuwa uwezo wa nguvu wa majini wa Uturuki utazidi ule wa meli ya kubebea ndege ya Ufaransa, ‘Charles de Gaulle’, mara tu meli mpya ya kitaifa ya kubebea ndege itakapozinduliwa.

Kwenye makala iliyochapishwa Jumanne, gazeti hilo liliashiria tangazo rasmi la Rais Recep Tayyip Erdogan kuhusu mradi wa National Aircraft Carrier wiki iliyopita katika maonesho ya TEKNOFEST — tamasha kubwa zaidi duniani la anga, na teknolojia.

Le Figaro liliutaja mradi huo kuwa “mradi mkubwa mno,” likieleza kuwa meli hiyo itakayojulikana kama MUGEM (kifupi cha Kituruki cha National Aircraft Carrier) itakuwa na urefu wa mita 285, upana wa mita 72 na uzito unaozidi tani 60,000.

Hivyo itazidi kwa uwazi Charles de Gaulle ya Ufaransa (mita 261 kwa urefu, tani 42,500), ambayo kwa sasa ndiyo meli kuu ya kivita ya Mediterania. Uturuki inalenga kuimarisha nguvu zake za baharini kupitia mradi huu mpya.

MUGEM inatarajiwa kuzinduliwa kati ya mwaka 2027–2028 na kuanza kutumika ifikapo 2030, ikiwa na uwezo wa kubeba ndege za kivita pamoja na ndege zisizo na rubani za kivita za kisasa (UCAVs).

Hii itakuwa meli ya kwanza ya kubebea ndege iliyobuniwa na kujengwa ndani ya Uturuki, hatua kubwa katika uwezo wa kikosi cha majini cha taifa hilo.

Uturuki kujiunga na ‘klabu ya kipekee’ ya meli za kubebea ndege

Mradi wa MUGEM unalenga kuimarisha uwepo wa Uturuki katika bahari ya Mediterania na pia katika ulingo wa kimataifa wa majini.

Le Figaro, ikiashiria matamshi ya Luteni Mhandisi Aykut Demirezen, ilisema kuwa meli hiyo itakuwa na uwezo wa kusafiri kati ya Uturuki na New York bila kujaza mafuta, kutokana na usanifu wa hali ya juu wa ‘haidrodinamiki’.

Makadirio yanaonyesha kuwa muundo wa meli utapunguza matumizi ya mafuta kwa takribani asilimia 1.5 na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.

Meli hiyo imeundwa kubeba takribani ndege 50, zikiwemo ndege za kivita na ndege zisizo na rubani.

Tofauti na meli za Magharibi, MUGEM itabuniwa mahsusi kwa ndege zisizo na rubani kuanzia mwanzo, zikiwemo KIZILELMA (ndege ya kivita isiyoonekana kirahisi kwenye rada, inayoweza kutua na kuruka kutoka melini) na ANKA 3, ndege isiyo na rubani ya kivita.

Pia itakuwa na uwezo wa kubeba HÜRJET, ndege ya juu ya mafunzo ya kivita yenye mwendo wa kasi wa juu kuliko sauti, na pia ndege nyepesi ya kivita, ambayo zaidi ya asilimia 80 ya vipengele vyake hutengenezwa ndani ya Uturuki.

Ripoti hiyo pia ilinukuu kauli za Rais Erdogan akibainisha kuwa meli hiyo mpya itazidi TCG Anadolu, meli ya kubebea ndege zisizo na rubani yenye urefu wa mita 231 na inayotumika sasa.

“Endapo ratiba itazingatiwa,” ripoti hiyo ilihitimisha, “Uturuki itaingia katika kundi la kipekee la mataifa yenye uwezo wa kutengeneza meli kubwa za kubebea ndege, kama Marekani, Urusi, Ufaransa na China.”

CHANZO:TRT World and Agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us