Mbuyu kutoka Kongwa, mkoani Dodoma, umeanguka.
Mbuyu kutoka Kongwa, mkoani Dodoma, umeanguka.
Aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Yustino Ndugai amefariki dunia Agosti 6, 2025 akiwa na umri wa miaka 62.
7 Agosti 2025

Ndugai ameaga dunia siku chache baada ya kushinda kura za maoni za kuwania nafasi ya jimbo la Kongwa, nafasi ambayo alikuwa aitetete kwa mara nyingine tena.

Ndugai, ambaye amekuwa mbunge wa jimbo la Kongwa kwa miaka 25, amehudumu nafasi mbalimbali ndani ya bunge la Tanzania, ikiwemo nafasi ya Unaibu Spika, kutoka mwaka 2010 hadi mwaka 2015.

Aliteuliwa kama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015 na kuhudumu nafasi hiyo hadi mwaka 2022.

Mwanasiasa huyo, mwenye stashahada ya wanyamapori kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika, maarufu kama MWEKA, atakumbukwa kwa misimamo yake dhidi ya wapinzani ndani ya bunge la Tanzania, ambapo mara kwa mara alitoa na kuwapa likizo ya lazima baadhi ya wabunge hao, akiwemo Tundu Lissu na John Mnyika.

Lakini atakumbukwa zaidi kwa hatua yake ya kujiuzulu nafasi ya uspika mwanzoni mwa mwaka 2022, na kuwa Spika wa kwanza aliye madarakani kujiuzulu kwa hiyari yake katika historia ya Bunge la vyama vingi nchini Tanzania.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Ndugai alinukuliwa akisema kuwa uamuzi huo kuwa umetokana na "uamuzi wake binafsi na uliozingatia na kujali maslahi mapana zaidi ya taifa, serikali na chama chake hicho".

Hata hivyo, wengi wanaona kwamba maamuzi yake yalitokana na kauli aliyoitoa wiki kadhaa nyuma, kuhusu mwenendo wa ukopaji wa serikali ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiifananisha na “nchi kuuzwa”.

Ndugai alionesha kukerwa na uchukuaji wa mikopo unaofanywa na Serikali ikiwemo trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani( IMF).

Katika majibu yake, Rais Samia alisisitiza kuwa serikali yake itaendelea kukopa kwa ajili ya kuleta maendeleo hata kama kuna watu wanatoa kauli za kukatisha tamaa.

Kufuatia mashinikizo kadhaa, Ndugai alilazimika kuomba msamaha kwa Watanzania, akisema  “nimekosa mimi nimekosa sana, nimekosa mimi Mungu anisamehe, Watanzania nisameheni, asanteni sana.”

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us