Serikali ya Uturuki kupitia Wizara yake ya Biashara imetangaza kuwa nchi yake na Syria zimefanikiwa kusaini Makubaliano (MoU) ya kuanzisha Baraza la Biashara la Pamoja linalolenga kurejesha ushirikiano wa taasisi kati ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yalitimia rasmi Jumatano wakati wa kikao kilichokuwa kinaongozwa na Waziri wa Uchumi na Viwanda wa Syria, Nidal Al-Shaar, pamoja na Naibu Waziri wa Biashara wa Uturuki, Ozgur Volkan Agar.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na wajumbe wa Bodi ya Mahusiano ya Kiuchumi ya Nje ya Uturuki (DEIK), ujumbe wa Syria, pamoja na viongozi wa biashara kutoka pande zote mbili.
Mchakato wa ujenzi upya wa Syria
Majadiliano yalijikita katika fursa za ushirikiano katika mchakato wa ujenzi wa Syria mpya baada ya vita, hususan katika maeneo ya miundombinu na huduma za umma kupitia mifumo ya Kujenga, Kuendesha na baadae Kukabadhi mradi (BOT) na Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
“Kwa lengo la kurejesha ushirikiano wa taasisi kati ya nchi hizi mbili, Makubaliano ya Kuelewana yamesainiwa kuanzisha Baraza la Biashara la Uturuki na Syria,” ilisema Wizara ya Biashara katika taarifa yake.
“Pia, makubaliano tisa ya ziada yamesainiwa kati ya mashirika ya kiraia kutoka pande zote mbili, ambayo yameweka msingi imara na endelevu wa ushirikiano.”
Wizara hiyo ilisisitiza kuwa Uturuki itaendelea na juhudi zake za kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya sekta binafsi za mataifa hayo, kwa lengo la kupanua na kuanzisha rasmi mahusiano ya kiuchumi na kibiashara.