Ndege aliye katika nembo zote za Taifa za Uganda, Korongo wa kijivu au ‘Gray Crested Crane’ ni ndege ambaye anatambulika kwa urembo wake.
Mwili wake wa kijivu unatofautiana sana na mabawa yake meusi na meupe, na pochi nyekundu inayong'aa kwenye koo.
Jambo la kuvutia zaidi, nguzo ya manyoya ya dhahabu huunda taji linalozunguka kichwa chake.
Wengi wanapatikana Uganda, na wengine nchini Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Msumbiji, Afrika Kusini na Zimbabwe.
Wakiwa na urefu wa takriban mita 1, wengi wao huishi katika maeneo ya ardhioevu - kingo za mito, karibu na mabwawa na nyanda za wazi - ambapo huzaliana na kula mbegu za nyasi, vyura wadogo, wadudu na wanyama wengine wasio na uti wa mgongo.
Si ndege wa kuhama hama ingawa wanaweza kufanya mienendo tofauti ya ndani ya maeneo yao kulingana na msimu na wingi na usambazaji wa chakula, maeneo ya viota na mvua.
Mara tu wanapokutana na wenzi wao, korongo wenye taji ya kijivu huwa na jike mmoja.
Wanajulikana kwa kucheza densi.
Wapenzi wakionekana mara kwa mara wakicheza pamoja na kusafisha safisha shingo ya mwenzao, ishara ya mapenzi.Korongo anaweza kuishi hadi miaka 14.
Hutaga mayai kati ya mawili hadi matano ambayo yanalindwa na korongo wote wa kike na wa kiume kwa siku 28-31.
Vifaranga wanaweza kuanza mwendo mara tu wanapoangualiwa, na huruka baada ya siku 56 mpaka100.Muda wa korongo kuzaliana ni wakati wa kiangazi, na wale walio kusini mwa Afrika wakati wa mvua.
Mara nyingi ndege hawa hukusanyika na kulala pamoja wakati wa usiku katika vikundi vya kati ya ndege 20 na 200.Korongo wa kijivu anaweza kuishi kati ya miaka 20 na 30.
Lakini ndege hawa wako hatarini. Kwa mfano katika miaka ya 1970, Uganda ilijivunia kuwa na zaidi ya korongo 100,000, lakini leo idadi hiyo inaripotiwa kupungua hadi kufikia 10,000, takwimu hizi ni kulingana na Shirika la Nature Uganda.
Watalamu wanasema sababu ya kupungua ni kuongezeka kwa idadi ya watu, mahitaji makubwa ya chakula yanayosukuma watu kulima katika maeneo oevu, na kuwaacha korongo bila maeneo yao ya asili.
Watu wengine wanataka kubadilisha matumizi ya ndege hawa na kuwafuga huku wengine wakiamini kuwa mayai na manyoya yao yana sifa za dawa.
Kuenea kwa ujangili na biashara haramu sio tu kwamba hupunguza idadi ya korongo, lakini pia huzuia korongo waliokomaa kutunza viota na vifaranga vyao.
Kwa upande wake, Uganda imeongeza ulinzi kwa ndege huyu na hata kupitisha sheria za kumlinda.
Mtu anaweza kupata kifungo cha maisha jela na/au faini ya zaidi ya dola milioni 5.6 (shilingi bilioni 20 za Uganda) akipatikana na hatia ya kuua korongo.