AFRIKA
3 dk kusoma
Marekani yasitisha huduma za viza nchini Zimbabwe
Ubalozi wa Marekani ulieleza hatua hiyo kuwa ya muda na ni sehemu ya juhudi za uongozi wa Trump za "kuzuia viza nyingi na matumizi mabaya."
Marekani yasitisha huduma za viza nchini Zimbabwe
Marekani imeweka vikwazo vya kutoa viza kwa nchi kadhaa barani Afrika/ Reuters
tokea masaa 5

Marekani imetangaza kusitisha maombi yote ya viza ya kawaida kwa raia wa Zimbabwe, ikiwa ni kikwazo cha hivi punde zaidi kwa wasafiri kutoka Afrika.

Wizara ya Mambo ya Nje ilisema Alhamisi kwamba Ubalozi wa Marekani nchini Zimbabwe utasitisha huduma zote za kawaida za viza kuanzia Ijumaa "huku tukishughulikia masuala hayo na Serikali ya Zimbabwe".

Hili limekuja siku chache baada ya Marekani kuzindua mradi wa majaribio unaowataka raia wa nchi nyingine mbili za Afrika, Malawi na Zambia, kulipa dhamana ya hadi $15,000 kwa viza ya utalii au biashara.

Dhamana itaondolewa ikiwa muombaji atasalia Marekani baada ya muda wa viza yake kuisha.

Ubalozi huo ulielezea hatua hiyo kuhusu Zimbabwe kuwa ya muda na ni sehemu ya juhudi za uongozi wa Trump za "kuzuia muda wa viza kuzidishwa na matumizi mabaya."

Viza nyingi za kidiplomasia na zile zilizo rasmi hazitoathiriwa, Marekani ilisema.

Vikwazo vya kusafiri

Marekani imetekeleza vikwazo vipya vya usafiri kwa raia kutoka nchi kadhaa za Afrika chini ya sera pana za uhamiaji za Rais Donald Trump, huku ikizishinikiza nchi za Kiafrika kuwakubali watu waliofukuzwa kutoka Marekani ambao si raia wao.

Mwezi Juni, Marekani iliweka marufuku ya kusafiri kwa raia kutoka mataifa 12, saba kati yao barani Afrika.

Iliweka vikwazo vilivyoimarishwa kwa mataifa mengine saba, matatu yakiwa ya Kiafrika. Marekani pia imezitaka nchi 36, nyingi kati yao zikiwa barani Afrika, kuimarisha uhakiki wao wa wasafiri au zikabiliane na marufuku kwa raia wao kutembelea Marekani.

Zimbabwe, Malawi na Zambia zote zilikuwa kwenye orodha hiyo ya nchi 36 zilizoombwa kuimarisha hati za kusafiria za raia wao na kuchukua hatua za kushughulikia hali ya raia wao ambao wako Marekani kinyume cha sheria.

"Uongozi wa Trump unalinda taifa letu na raia wetu kwa kuzingatia viwango vya juu zaidi vya usalama kwa taifa na usalama wa umma kupitia mchakato wetu wa viza," Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema Alhamisi.

Dhamana ya viza

Sera mpya ya dhamana iliyotangazwa Jumanne inawahitaji raia wa Malawi na Zambia kulipa dhamana za $5,000, $10,000 au 15,000 kama sehemu ya maombi yao ya viza ya kitalii au ya biashara kwenda Marekani.

Chini ya mpango huo, raia wa nchi hizo lazima pia wafike na kuondoka katika mojawapo ya viwanja vya ndege vitatu: Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Boston Logan, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK wa New York au Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles karibu na Washington D.C.

Mpango wa majaribio wa dhamana ya viza utaanza kutekelezwa Agosti 20, Wizara ya Mambo ya Nje ilisema.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us