Kambi za wakimbizi katika eneo la Gambella nchini Ethiopia zinakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu kufuatia kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa ambayo imelemaza huduma muhimu, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa chakula, huduma za afya, na kukabiliana na magonjwa.
Kambi hiyo iko kusini-magharibi mwa Ethiopia karibu na mpaka wa Sudan Kusini.
“Gambella imehifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wengi wa Sudan Kusini tangu 2014. Leo, zaidi ya wakimbizi 395,000 wanaishi katika kambi saba,” Shirika la Médecins Sans Frontières (MSF) limesema.
Kupungua kwa kasi kwa usaidizi wa kibinadamu, kutokana na kupunguzwa kwa ufadhili wa kimataifa kutoka kwa wafadhili wakuu kama vile USAID, tayari kumelazimisha kusimamishwa kwa mipango ya lishe.
“Lishe imesimamishwa katika kambi nne kati ya saba za wakimbizi, na kuacha karibu watoto 80,000 walio chini ya umri wa miaka mitano katika hatari ya utapiamlo unaotishia maisha.”
Wakimbizi wanalalamika kuwa hawana mahitaji ya kutosha.
"Tunapokea chakula mara moja kwa mwezi-mahindi, ngano, na mtama-lakini kila mara huisha kabla ya mwezi kuisha," alisema Nyauahial Puoch, mama wa watoto watano ambaye binti yake mwenye umri wa miezi 17 alilazwa katika kituo cha lishe cha wagonjwa cha MSF huko Kule. "Baadhi ya vitu tulivyokuwa tukipata havitolewi tena."
Tangu Oktoba 2024, wakimbizi katika kambi ya Kule wameripotiwa kupokea kalori 600 kwa siku—chini ya asilimia 30 ya kiwango cha chini kinachopendekezwa.
Usambazaji wa chakula katika kambi nyengine pia umetatizwa, huku nyengine zikienda kwa miezi bila kufanya kazi kwa sababu ya masuala ya ugavi na upungufu wa fedha. Athari kwenye lishe ya watoto ni kubwa.
MSF iliripoti ongezeko la asilimia 55 ya watoto wanaolazwa katika mpango wake wa lishe ya matibabu mwaka huu ikilinganishwa na 2024.
Nusu ya kesi hizo zilitoka nje ya kambi ya Kule, na hivyo kusisitiza ukubwa wa kuzorota kwa kanda.
Huduma ya afya imepungua
Upatikanaji wa huduma za afya pia umezidi kuwa mgumu kwani mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali yamejiondoa katika eneo hilo. Idara ya wagonjwa wa nje ya MSF huko Kule ilirekodi ongezeko la asilimia 58 ya wagonjwa mwaka huu, wakati kwa wajauzito iliongezeka kwa asilimia 72 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
"Tunapokea wagonjwa zaidi kutoka kambi nyingine kwa sababu huduma nyingi za afya hazipatikani tena ndani ya nchi," alisema Armand Dirks, mratibu wa mradi wa MSF huko Gambella. "MSF imezidiwa, na tunahofia idadi itaendelea kuongezeka."
Licha ya kujiendesha kwa uwezo kamili, MSF ilisema rasilimali zake bado hazitoshi kukidhi mahitaji yanayokua. Inahimiza serikali kuchukua hatua kuelekea kujumuisha idadi ya wakimbizi katika mifumo ya afya ya kitaifa na kuimarisha huduma za umma ili kuhimili upungufu wa misaada kwa siku zijazo.
"Bila ya hatua za haraka kutoka kwa mamlaka ya kitaifa na washirika wa kimataifa, tatizo hili litaendelea kuongezeka, na kuweka maelfu ya watu katika hatari kubwa," Birhanu alisema.
Mwezi Februari, mlipuko wa kipindupindu katika eneo la Gambella nchini Ethiopia uligharimu maisha ya watu 14, huku zaidi ya kesi 200 zikiripotiwa.
Kufikia Aprili, idadi ya kesi zilizoripotiwa ilikuwa imeongezeka hadi kufikia 2,016, na vifo 32.
Eneo hilo lilikuwa likikabiliwa kwa wakati mmoja na malaria, likirekodi kiwango cha juu zaidi cha matukio nchini kote mwezi Aprili - kesi 462 kwa kila watu 100,000 - kulingana na Kitengo cha afya cha Ethiopia.