Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameridhishwa na msimamo wa Senegal dhidi ya udhalimu unaofanywa na Israel, akisema kuwa mshikamano wao na watu wa Palestina ni wa kupigiwa mfano.
“Mapambano yetu yanaendelea mpaka mauaji ya kimbari ya Gaza yanaisha na wale wenye kuwauwa watoto wasio na hatia kwa njaa wanawajibishwa," alisema Erdogan katika mkutano wa pamoja na wanahabarI akiwa na Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane siku ya Alhamisi.
Erdogan aliuelezea uhusiano kati ya Uturuki na Senegal kama wa kindugu, na wenye kuendelea.
Kulingana na Erdogan, majadiliano ya Alhamisi yaliangazia fursa za ushirikiano katika uwekezaji, biashara, usalama na ulinzi, mapambano dhidi ya ugaidi, uchimbaji madini, usafiri, uvuvi na nyanja nyinginezo.
Rais huyo wa Uturuki alibainisha kwamba, Ankara inalenga kuongeza ujazo wa kibiashara hadi Dola Bilioni 1 na hatimaye Dola Bilioni 3.
Kwa upande, Sonko aliipongeza Uturuki kwa misaada yake endelevu, akiiita nchi hiyo kama taifa ndugu.
Sonko alimshukuru Erdogan kwa kuwa moja ya viongozi wachache duniani wenye kupinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.
"Tunafurahishwa na namna ndugu zetu wanavyovutiwa na bidhaa za ulinzi za Uturuki. Tunatazamia kuimarisha mshikamano kwenye eneo hili katika siku zijazo," alisema.
'Kupinga dharau'
Katika miaka ya hivi karibuni, Uturuki imezidi kujiimarisha barani Afrika, katika kipindi ambacho mataifa mengi ya Afrika yamewapa kisogo waliokuwa watawala wao.
Ankara imetia saini makubaliano kadhaa ya kiulinzi na nchi mbalimbali zikiwemo Somalia, Libya, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Nigeria na Ghana.
Mikataba hiyo imefungua fursa za bara la Afrika, kwa watengenezaji wa bidhaa za kiulinzi.
Erdogan alilieleza bara la Afrika kama “nyota yetu ya karne" kutokana na utajiri wake rasilimali ya vijana na uzuri wa asili.
"Hakuna taifa lenye maono linaloweza kulidharau bara la Afrika," alisema.
Kulingana na Erdogan, yeyote mwenye kukosoa uhusiano wa Uturuki na Afrika alikuwa “akiizamisha nchi yetu kwenye maji".
"Tunakataa kila aina ya dharau kwa bara la Afrika,” aliongeza.