Baraza la Mawaziri nchini Uganda limeidhinisha kufutwa kwa Sheria ya Kituo cha Mafunzo ya Sheria (LDC), na kufikisha ukomo wa ukiritimba wake wa miongo kadhaa kwenye shahada ya mafunzo ya uanasheria.
Kwa miaka 55 kituo hiki ndicho kilikuwa na uwezo pekee nchini Uganda kutoa mafunzo ya ubobezi wa uanasheria na idhini ya kuwa wakili.
Hatua hiyo inafungua milango kwa taasisi zilizoidhinishwa na shule za sheria nchini kote kutoa mafunzo hayo, na hapo kuongeza watu wengi zaidi kupata elimu hiyo ya sheria.
Sasa Kituo cha Taifa cha Mitihani ya Sheria kitaundwa kiwe chombo cha kusimamia mafunzo na mitihani sanifu kwa Kozi ya Wanasheria katika taasisi zote zilizoidhinishwa.
“ Kituo cha kitaifa cha mitihani ya sheria kitatayarisha mtihani mmoja kutoka kwa hatua ya diploma ya masuala ya sheria,” LDC imethibitisha katika taarifa.
Kituo cha LDC kimesitisha kuwasajili wanafunzi kwa Kozi ya Wanasheria wa 2025, kutokana na vikwazo vya miundombinu na wafanyakazi.
Mawakili sasa itabidi wasubiri kwa mwaka mmoja, maandalizi, na kutokuwa na uhakika wakati taifa linapoelekea kwenye mfumo wa kimapinduzi wa mafunzo ya sheria.
Ili kudhibiti usajili wa siku zijazo na kudumisha ubora, LDC imeanzisha mtihani wa lazima wa kabla ya kuingia kwa usajili wa 2026.
Imesema miongozo, ikijumuisha tarehe za mitihani na vigezo stahiki, vitachapishwa kufikia Septemba 1, 2025, kupitia magazeti ya taifa na mitandao ya kijamii ya LDC.
Marekebisho hayo yanaashiria mabadiliko katika mfumo wa elimu ya sheria nchini Uganda. Kwa kufanya ugatuzi wa mafunzo na kuanzisha mtihani wa kitaifa wa pamoja, Kituo cha Kitaifa cha Mitihani ya Kisheria kinalenga kutatua masuala ya msongamano na kutofikiwa kwa urahisi kwa kituo hicho.
Sasa kuna wanafunzi 3000 katika kituo hicho, je ni mwongozo gani wanapata huko? Hakuna. Hivyo hakuna haja tuseme mafunzo yenye tija yanatolewa huko.Sioni haja,” alisema Jaji Irene Mulyagonja, mwenyekiti wa Baraza la Sheria la Uganda.
“ Ikiwa una wasiwasi kuhusu ubora, hii inategemea uzoefu wa kazi bora. LDC sasa ina lengo la kufanya mafunzo haya yapatikane katika vituo vingine,” Waziri wa Sheria Nobert Mao amesema.