AFRIKA
2 dk kusoma
Jamii forums yafungiwa kwa siku 90 kwa 'kudhalilisha serikali na Rais' wa Tanzania
Aidha TCRA imeongeza kuwa maudhui hayo yanakinzana na mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania, hivyo kuhatarisha mshikamano wa kitaifa, amani na taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jamii forums yafungiwa kwa siku 90 kwa 'kudhalilisha serikali na Rais' wa Tanzania
TCRA inashutumu Jamii forums kuchapisha habari zinazodhalilisha Rais wa Tanzania / Others
6 Septemba 2025

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA amesitisha kwa muda wa siku 90, leseni ya huduma za maudhui mtandaoni iliyotolewa kwa kampuni ya Vapper Tech Limited, wamiliki wa jukwaa la Jamii Forums.

Jamii Forums inashutumiwa kuwa, kupitia mitandao yake imechapisha maudhui ya kupotosha umma, kukashifu na kudhalilisha Serikali pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika notisi iliyochapisha kwenye mtandao wake wa X, TCRA ilisema kuwa taarifa hizo inazodai kuwa potofu zilichapishwa mnamo Septemba 04, 2025 na kubainisha kwamba yamekiuka Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2022 na 2025.

"TCRA inapenda kuufahamisha umma kuwa, pamoja na kukiuka kanuni, maudhui hayo yanakinzana na utamaduni, mila na desturi za Kitanzania, jambo linaloweza kuathiri umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, na pia kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," —imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha TCRA imeongeza kuwa maudhui hayo yanakinzana na mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania, hivyo kuhatarisha mshikamano wa kitaifa, amani na taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa mtandao wa Jamii forums, taarifa hizo zinahusiana na kuchapisha taarifa ya Mwanasiasa Humphrey Polepole kuhusu Rostam kumiliki mgodi wa makaa ya mawe kwa asilimia 70 na taarifa za uhusiano kati ya Rais wa Tanzania na "Mfanyabiashara" Wicknell Chivayo bila kuzingatia mizania.

‘‘Kwa mujibu wa TCRA, JamiiForums ilishindwa kutafuta maoni ya Mamlaka husika/Msemaji wa Rais/Serikali, kuthibitisha uhalisia wa picha (za Rais na Chivayo) zilizotumika, na hivyo kuuaminisha Umma taarifa za upande mmoja,’’ iliandika Jamii forums katika mtandao wake wa X.

Adhabu hiyo ya TCRA inaanza kutumika leo Jumamosi, Novemba 6 kwa muda wa siku 90.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us