Ukifika nchini Madagascar bila shaka hautatoka bila kuangalia sanaa maalumu inayoitwa Hiragasy.
Nchi hii iko nje ya pwani ya kusini-mashariki mwa Afrika, ni kisiwa cha nne kwa ukubwa duniani, nchi ya kisiwa cha pili kwa ukubwa.
Hiragasy ni maonyesho yanayojumuisha nyimbo, ngoma na hotuba.
Ikiwa na asili ya jamii za kutoka katika nyanda za juu za kati ya Madagascar, sanaa hii huonyeshwa katika maeneo ya umma.
Kwa ujumla, uhusisha vikundi viwili vya watu na huchukua muda wa saa moja na dakika thelathini, kufuata muundo wa kawaida, ikiwa ni pamoja na ngoma, salamu, simulizi, ngoma na nyimbo za asili.
Tamaduni hii inaripotiwa kuanza mwishoni mwa karne ya 18 wakati mwana wa mfalme alipowatumia wanamuziki kwa mara ya kwanza kuteka umati kwa hotuba zake za kisiasa.
Watazamaji wana jukumu kubwa katika hafla za hiragasy, wakionyesha kuridhika au kutoridhishwa kwao na talanta ya washiriki wa kikundi na ujumbe wanaotangaza kupitia shangwe, au sauti tofauti.
Maneno ya maonesho ya hiragasy yanarejelea maadili, uraia na utamaduni, na muziki unaimbwa kwa kutumia ala za kitamaduni. Hiragasi iko katika sherehe na hafla zote za kitamaduni za Kimalagasi.
Hiragasy ni utambulisho wa kitaifa na hurithishwa ndani ya familia, watoto wakiwafuata wazazi wao kwenye ziara na kujumuika kwenye maonesho.
Wakati wa enzi ya kifalme, hiragasy ilitumiwa kama njia ya mawasiliano kati ya watawala na watu ili kuwasilisha ujumbe.
Baada ya dini ya Kikristo kuingia nchini humo, sanaa hii ilitumika kama njia ya kueleza imani na utamaduni wa Kimalagasi zaidi ya mahekalu.
Leo, inatazamwa kama njia ya kuwasilisha maadili ya kitamaduni, historia na ujuzi wa mababu wa Malagasy.
Katika maeneo ya vijijini, hiragasy inachukuliwa kuwa njia muhimu ya kuelimisha vijana. Inadumisha mshikamano wa kijamii na kukuza amani ndani ya familia na kati ya raia na jamii.