Sudan Kusini inakabiliwa na changamoto ya mapato huku jirani yake Sudan akiamua kufunga kituo kikuu cha mafuta.
Wizara ya Nishati na Petroli ya Sudan imeamuru kufungwa kwa dharura kwa vituo vya mafuta katika eneo la Heglig karibu na mpaka na Sudan Kusini kufuatia shambulio la ndege isiyo na rubani mapema Jumamosi.
Shambulio hilo, lililolaumiwa kwa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), lililenga Kambi ya Operesheni ya Heglig karibu saa mbili na nusu asubuhi, na kuharibu kituo cha uwanja wa ndege na kusababisha kuhamishwa kwa wafanyakazi, kulingana na barua ya Wizara ya Agosti 30.
Uwanja wa ndege haujafanya kazi tangu Aprili 2023.
Uamuzi wa serikali ya Sudan kama ilivyoelezwa katika barua yake, unafuatia sababu za kiusalama ikiwemo mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yanayohusishwa na Vikosi vya Rapid Support Forces, RSF.
Vikosi vya serikali vimekuwa vikipambana na RSF tangu Aprili 2023.
Hii si habari njema kwa jirani yake Sudan Kusini ambayo kwa asilimia kubwa, inategemea miundombinu ya Sudan katika uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ghafi kupitia Bahari Nyekundu.
Kituo cha mafuta cha Heglig kinachofungwa kiko kando ya mpaka kusini mwa Sudan na ni kituo kikuu cha usindikaji wa mafuta ya Sudan Kusini. Uzalishaji wa mafuta ni tegemeo kuu la mapato kwa Sudan Kusini.
Kabla ya mzozo kuanza nchini Sudan 2023, Sudan Kusini ilikuwa ikituma kati ya mapipa 100,000 na 150,000 ya mafuta kwa siku kupitia Sudan kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Kufungwa kwa mabomba ya Heglig kunatarajiwa kuathiri uzalishaji katika maeneo ya mafuta ya Unity nchini Sudan Kusini na mtiririko mzima wa mafuta. Sudan Kusini kwa sasa inauza nje takriban mapipa 110,000 ya mafuta kwa siku na inapata mapato mengi ya serikali kutokana na mafuta hayo.
Kusimamishwa kwa mauzo ya nje kunaweza kuzidisha mzozo wa kiuchumi wa nchi na kuzidisha hali mbaya ya kisiasa.
Hatua hii inakuja wakati ambapo usafirishaji wa mafuta ulikuwa umeanza tena Januari baada ya kusimamishwa kwa karibu mwaka mmoja kutokana na uharibifu wa awali wa bomba uliosababishwa na mapigano nchini Sudan.
Tayari Bunge la Taifa la Sudan Kusini linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha, ambapo limeitaka serikali kujieleza kwa nini hakuna pesa.
Wabunge wana wasiwasi kwamba watumishi wa umma wanalazimika kupanga foleni kwa saa kadhaa katika benki ili kutoa pesa za kujikimu.
Kwa sasa hatma ya Sudan Kusini kijikwamua kiuchumi inategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa hali ya usalama kutoka kwa jirani yake Sudan.