Adha ya kutafuta matibabu nchini Afrika Kusini
AFRIKA
3 dk kusoma
Adha ya kutafuta matibabu nchini Afrika KusiniKulingana na Taasisi ya kimataifa ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), uwepo wa wanachama wa “Operation Dudula”, umefikia zaidi ya nusu ya vituo vya afya 15 katika maeneo yaliyoathiriwa.
Wanawake wakimbizi wakisubiri huduma kwenye kambi ya wakimbizi ya Musina ya nchini Afrika Kusini./Picha:MSF
tokea masaa 16

Safari za kila wakati za hospitali hazikuwa za kaiwada kwa Ndlovu*, mwanamke mjamzito kutoka Zimbwabwe ambaye kwa sasa anaishi katika jimbo la Gauteng nchini Afrika Kusini.

Kutokana na hali yake ya kiafya, Ndlovu hapaswi kuwa katika msongo wowote wa mawazo.

Hata hivyo, anapokaribia kujifungua, Ndlovu anakabiliwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali yake ya kiafya, kama ilivyo kwa raia wengine wa kigeni nchini Afrika Kusini.

Katika moja ya safari zake hospitalini, Ndlovu alisikia maneno “Operesheni Dudula”, neno maarufu kwa jamii ya Wazulu, lenye kumaanisha “kung’oa”.

Hili ni neno ambalo limejizoelea umaarufu sasa kwenye sekta ya afya, hususani kwenye maeneo ya Gauteng na KwaZulu-Natal.

"Rafiki yangu mmoja aliniambia namna wageni walivyokuwa wakifukuzwa mahospitalini, tulikuwa tunakesha tukiomba jambo hilo lisitutokee. Mara ghafla, kikundi cha watu kikavamia hospitali tuliyokuwemo na wakafanya kitu kile kile," anasema Ndlovu katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Majibu kutoka taasisi husika

Hata hivyo, kumekuwepo na matumaini baada ya taarifa za kukamatwa kwa baadhi ya wanakikundi cha Dudula na taarifa iliyotolewa na taasisi ya kupinga ubaguzi iitwayo Kopanang Africa (KAAX).

"Ubaguzi sio suluhi ya kupatikana kwa huduma. Ni ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu. Tusambaze ujumbe huu," ilisomeka taarifa ya taasisi hiyo kutoka ukurasa wake wa X.

Maandamano ya kikundi cha Operesheni Dudula, yaliyofanyika nje ya hospitali ya Kalafong miaka mitatu iliyopita, yalimlazimu rais Cyril Ramaphosa kutoa msimamo wa nchi yake.

"Vitendo kama hivi havitovumilika,"alisema Ramaphosa.


Kulingana na wachambuzi mbalimbali, janga hilo linasisitiza umuhimu wa kukabiliana na changamoto ya utoaji wa huduma za afya kwa watu wageni.

Janga kubwa

Kulingana na Taasisi ya kimataifa ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), uwepo wa wanachama wa “Operation Dudula”, umefikia zaidi ya nusu ya vituo vya afya 15 katika maeneo yaliyoathiriwa.

Mtaalamu wa masuala ya mawasiliano wa MSF Jane Rabothata, anaelezea hali ya isiyoridhisha kwenye vituo vingi vya afya nchini humo.

"Hii ni kutokana na sababu ya watu kufukuzwa kutoka kwenye vituo hivyo vya afya," anasema.

Katika moja ya picha mjongeo zilizosambaa mtandaoni, raia mmoja wa Congo anaonekana akiwasihi wanachama wa Dudula wamruhusu ndugu yake mwenye changamoto ya kuona, apate huduma ya afya.

"Nyamaza na uondoke eneo hili,” alisikika akiambiwa.

Suala la haki

Shirika la MSF limetahadharisha kuwa vitendo vya kuwanyima wageni huduma za afya zinaweza kuathiri mfumo mzima wa sekta ya afya.

"Katiba yetu inaruhusu mtu yeyote yule kupata huduma za afya bila kuangalia wanatokea wapi," Rabothata anaeleza.

Shirika hilo limetaka polisi wa nchi hiyo kutoa ulinzi kwa taasisi zilizoathirika.

Suala hili, pia limepewa uzito na wabunge wa nchi hiyo.

Makhi Feni, mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Elimu, amekosoa operesheni ya Dudula.

"Matendo haya hayana maana yoyote. Watu hawaji Afrika Kusini kwa matashi yao tu, wanakuja kutafuta chakula,"Feni anasema.

Mbunge huyo, anaelezea wasiwasi na mpango wa kikundi cha Dudula kulenga shule, ifikapo mwaka 2026, akionya kuwa vitendo hivyo vinakwenda tofauti na tunu za taifa hilo.

Mahangaiko ya kila siku

Uzoefu wa Ndlovu unaakisi yale yanayofanywa na kikundi cha Dudula.

Mmoja ya wanachama wa kikundi hicho hutembelea hospitali nchini humo na kuanza kuwauliza wagonjwa, akiwa ameshikilia cheti chake cha uraia wa Afrika Kusini.

"Kisha hutuambia kama yupo kati yetu ambaye hana cheti kama hicho, basi atoke nje ya hospitali,” anasema mama huyo mtarajiwa kutoka Zimbabwe.

"Nimekuja kugundua kuwa niko katika hatari ya kupoteza maisha iwapo mimi si raia wa Afrika Kusini. Niliamua kuondoka hospitalini hapo japo nilienda kwa uchunguzi," anasema.

Hata hivyo, Ndlovu hajakata tamaa. Bado ana matumaini ya kupatikana kwa maridhiano kati ya wazawa na raia wa kigeni waishio Afrika Kusini.

"Sisi ni kitu kimoja, tupendane. Tusaidiane mmoja wetu anapopatwa na matatizo," anasema.

 


CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us