Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika ametoa rambirambi zake kwa serikali ya Sudan kufuatia maporomoko ya ardhi huko Kaskazini mwa nchi hiyo.
Maporomoko ya ardhi yameangamiza kijiji cha Tarasin katika jimbo la Darfur nchini Sudan, na kuua takriban watu 1,000 katika moja ya maafa mabaya zaidi ya asili katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo.
Maporomoko ya ardhi yalitokea Jumapili baada ya siku kadhaa za mvua kubwa katika Milima ya Marrah, safu ya mbali ya volkano huko Darfur ya Kati.
“Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ameelezea kwa masikitiko makubwa kuhusu maporomoko ya ardhi yaliyotokea tarehe 31 Agosti katika kijiji cha Tarasin, Jimbo la Darfur Kaskazini, ambayo yameripotiwa kupoteza maisha ya zaidi ya watu 1,000,” taarifa kutoka Tuem ya AU imesema.
Inaripotiwa ni mtu mmoja tu aliyenusurika.
“Mwenyekiti wa Tume anatoa salamu za rambirambi kwa familia zilizofiwa na kutoa pole kwa wananchi wa Sudan waliofikwa na msiba huu. Mawazo yake pia yanaenda kwa mtu mmoja pekee aliyeokoka, ambaye uimara wake unaamasisha heshima na matumaini,” taarifa ya AU imesema.
Picha zinaonyesha manusura wakitafuta miili kwenye vifusi.
Janga hili linakuja huku vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vikiendelea kupamba moto tangu Aprili 2023.
Sehemu kubwa ya Darfur imesalia kutopewa msaada, huku makundi kama vile Madaktari Wasio na Mipaka yakionya kuhusu kuporomoka kabisa kwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.