Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema Mto Nile wa Ethiopia yaani Blue Nile, ambao hutoa hadi asilimia 86 ya maji ya Nile, kwa karne nyingi umechukua sio tu ardhi yenye rutuba ya nchi hiyo lakini pia dhahabu yake, na kuiacha Ethiopia bila faida.
Katika hotuba yake kupitia runinga Jumatatu usiku, siku chache kabla ya uzinduzi unaotarajiwa wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD), Abiy alifichua kuwa katika uchimbaji kwenye bwawa hilo kulipatikana "mabaki ya dhahabu kwenye mchanga uliokusanywa."
"Hii inazidisha majuto kwamba Mto Nile umekuwa ukichukua sio ardhi yetu tu, bali pia dhahabu ya Ethiopia kutoka kwenye milima yetu," Waziri Mkuu Ahmed alisema.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa Ethiopia imepata kutambuliwa kwa kiasi kidogo sana kwa kulinda utajiri wake wa asili.
“Sijawahi kusikia mtu akisema, ‘Uishi maisha marefu, miaka yako iwe mingi, kwa sababu yako tumepata haya,’ baada ya udongo wetu, dhahabu, samaki, magogo na miti yetu kuchukuliwa, badala yake, tulichosikia ni hasira na dharau kwamba tunatetea na kulinda mali zetu,” alisema.
Ethiopia imekuwa na mvutano na Misri kwa ujenzi wa bwawa lenye ukubwa wa megawati 6000, huku Misri ikisisitiza kuwa maji ya Mto Nile hayafai kutumika kwani mtiririko kwenda kwake utapungua.
Misri inategemea maji ya Mto Nile kwa kilimo na matumizi na inashikilia maamuzi yaliyofanywa na Uingereza wakati wa ukoloni.
Hata hivyo, Ethiopia na nchi nyengine zinazotumia maji haya zinasisitiza kuwa maazimio ya wakati wa ukoloni yapepitwa na wakati.
Ethiopai na misri zimeunda kamati za kujadili suala hilo.
Abiy alibainisha kuwa GERD, inayotarajiwa kuzinduliwa katika siku zijazo, imepata maji ya ziada kwa nchi za chini ya mto. Alitupilia mbali wito wa Ethiopia kuzuia mtiririko wa mto kabisa.
"Wengine husema, 'Zuia maji; yazuie kutiririka chini ya mto,' lakini hii si nia yetu, wala haiwezekani kuzuia maji kabisa," alisema.
Kulingana na Waziri Mkuu bwawa la GERD kwa sasa lina mita za ujazo bilioni 74, au lita trilioni 74, za maji, zinazotolewa kupitia mitambo na njia za kumwagika.
"Hatuna nia ya kuhifadhi maji zaidi ya yaliyoundwa; hata kama tungetaka, bwawa halingeweza kushikilia," alisema, akiongeza kuwa Ethiopia bado haijatumia na kujitosheleza kwa sehemu yake nzuri ya Blue Nile.