Katika moja ya mabwawa mjini Lagos, makao makuu ya kibiashara nchini Nigeria, Emeka Chuks-Nnadi anatizama maji.
Anatizama wanafunzi wake wakiingia kwenye bwawa mmoja baada ya mwingine. "Usipambane na maji. uwe unaelea tu. Jiachie. Maji yanakuhitaji," anawaambia watoto, huku akifuatilia hatua zao zote.
Leo hii, anawafunza kuelea juu ya maji. Wakati mvulana mwenye ulemavu wa macho anapomakinika kwenye maji, kocha anafurahia na kuona fahari.
Emeka, anafurahia nyakati kama hizi. Pia wanaeleza kwa nini alianzisha ‘‘Swim In 1 Day Africa’’ mwaka 2022, shirika la hisani lenye kufunza watoto wenye ulemavu kuogelea na usalama wa maeneo ya maji.
"Lengo langu ni kugeuza hofu na kufanya kuwa uhuru kwa watoto, hasa wale wanaoishi na ulemavu," ameiambia TRT Afrika.
Muelekeo wa maisha
Emeka hakuwa anataka kufanya kazi hii. Alikuwa na kampuni yake ya masuala ya utalii mjini Barcelona, Hispania, akiwa na wafanyakazi zaidi ya 150. Biashara ilikuwa inaendelea vizuri hadi wakati UVIKO-19 ulipoaathiri dunia 2021, na kutatiza biashara kabisa.
"Ugonjwa huo ulinipa mimi muda wa kutembelea Nigeria kwa miezi mitano 2021, na ziara hiyo ikabadilisha kila kitu," anakumbuka Emeka.
Yeye mwenyewe alianza kuogelea akiwa na umri wa miaka tisa baba yake akimfundisha wakati huo, "alikuwa muogeleaji mzuri sana" ambaye alitaka kurithisha familia yake kipaji hicho.
Mama yake Emeka alikuwa chachu ya yeye kupenda kusaidia, kila mara akimpeleka kuwatembelea watoto wenye ulemavu katika vituo vya kulea watoto.
"Kila mara mama yangu alikuwa akitufunza kuwa watu wenye furaha maishani, lazima uchukulie watu wote sawa, na unatakiwa uwapende na kuwainua watu wote walio karibu na wewe," anasema.
Ratiba ya Emeka inakwenda zaidi ya kufunza watu mbinu za kuogelea.
"Ajali nyingi za kuzama zinatokea kwa sababu watu hawaelewi namna ya kuolea juu ya maji. Ukiwa na hofu, viungo vyako vya mwili vinashtuka na unazama. Tunafundisha watu namna ya kutulia na kuwa salama," alieleza.
Huku ufadhili ukiwa bado ni changamoto, Emeka anaendelea kuongeza mbinu zingine katika mafunzo yake. Mipango yake anataka kutunga wimbo wa taifa kwa waogeleaji shuleni, ukiwa na miongozo ya usalama inayoendana na mziki.
"Katika kazi zote duniani, hii inaniridhisha sana. Mabadiliko yanafanyika ukiyaona. Unampa mtu mafunzo ya kuokoa maisha yake, na huwezi kufananisha hicho na kitu chochote," Emeka ameiambia TRT Afrika.
Egbon Oluwafemi, mwenye umri wa miaka 16, ni miongoni mwa wale ambao maisha yake yamebadilika.
"Baada ya kupata ajali, nilitengwa na watu; hakuna mtu aliyetaka kucheza na mimi, na nilikuwa tu mwenyewe nyumbani," anakumbuka.
"Niliona watu waliokuwa kwenye kambi ya uogeleaji kama fursa ya kuwa na furaha tena. Tangu nilipoanza, maisha yangu yamebadilika. Najihisi kama shujaa. Nahisi nimepata mafanikio makubwa sana. Naogelea baharini kwa saa tatu bila kupumzika."
Segun Vidal, 19 na mwenye ulemavu wa macho, pia ana matarajio makubwa zaidi. "Uogeleaji umenipa mimi uhuru na kufanya nijiamini. Nafanya mazoezi kwa ajili ya Olimpiki ya walemavu 2028 huko Los Angeles," alisema kijana huyo.