Viboko wasiopungua 50 na wanyama wengine wakubwa ndani ya hifadhi ya taifa ya Virunga iliyoko katika eneo la mashariki mwa DRC, wameripotiwa kufa kutokana na sumu ya kimeta, msimamizi wa mbuga hiyo alisema siku ya Jumanne.
Kulingana na muhifadhi wa eneo hilo Emmanuel De Merode, vipimo vilivyochukuliwa vimethibitika kuwa ni sumu ya kimeta. Chanzo cha sumu hiyo ambayo pia imesababisha kifo cha nyati mmoja bado hakijajulikana.
Picha zilizosambazwa na wasimamizi wa hifadhi hiyo, zilionesha miili ya viboko ikiwa inaelea juu mto Ishasha, huku mingine ikiwa imekwama kwenye matope.
Vifo hivyo vimesababisha hasara kubwa kwa hifadhi hiyo, ambayo, kwa miaka ya karibuni, imejizatiti kuongeza idadi ya wanyamapori haom hususani baada ya kupungua kwa idadi yao kutoka 20,000 hadi mamia kadhaa kufikia mwaka 2006. Kwa sasa, hifadhi ya Virunga ina viboko wapatao 1,200.
Kaa mbali na wanyamapori
Askari wa hifadhi ndani ya hifadhi hiyo, waliona tatizo pale walipoanza kushuhudia idadi kubwa ya wanyama waliokufa siku tano zilizopita katika mto huo, ambao unaunganisha mpaka wa Congo na Uganda na mkondo wake unapita kwenye eneo linalodhibitiwa na wapiganaji waasi.
Kimeta ni ugonjwa hatari sana unaotokana na bakteria ambao wanapatikana ardhini.
Wanyamapori wanaweza kuambukizwa kimeta kutoka sehemu ya ardhi, mimea au maji.
Katika taarifa siku ya Jumanne, taasisi ya kuhifadhi mazingira ya Congo ilionya wakazi wakae mbali na wanyamapori na kuchemsha maji yanayotoka kwenye vyanzo vya maji vya eneo hilo kabla ya kunywa.
De Merode alisema kuna maafisa ambao wako kwenye eneo la tukio na walikuwa wanajaribu kuwatoa viboko hao ndani ya maji kwa ajili kuwazika, lakini tatizo kukosekana kwa matinga ya kuwabeba.
Wanyama zaidi
"Ni vigumu kufika katika eneo hilo," De Merode aliiambia Reuters. "Tuna uwezo wa kupunguza kusambaa kwa maambukizi kwa kuwazika na magadi."
Mkondo wa mto huo unaelekea hadi Ziwa Edward, ambapo viboko zaidi walionekana wakiwa wamekufa.
"Kuna zaidi ya miili 25 ya viboko juu ya ziwa, kutoka Kagezi hadi Nyakakoma," Thomas Kambale, kiongozi wa shirika moja la kiraia huko Nyakakoma, ameiambia Reuters.
Tangu kuanza kwa vita vya wenyewe mwanzoni mwa karne hii, mbuga ya Virunga imeathirika sana kutokana na wapiganaji kuweka kambi humo.