Uturuki itaweka msingi siku ya Ijumaa wa mradi mkubwa wa reli sehemu ya mashariki mwa nchi ambao utakuwa sehemu ya mkakati wa ushoroba wa Zangezur, njia muhimu katika eneo la mataifa ya Caucasus ya Kusini.
Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu Abdulkadir Uraloglu ametangaza Alhamisi kuwa njia ya reli ya Kars-Igdir-Aralik-Dilucu, ambayo ni kilomita 224, itakuwa ushoroba muhimu, utakaounganisha Azerbaijan na eneo la Nakhchivan.
Inatarajiwa kubeba abiria milioni 5.5 na mizigo tani milioni 15 kila mwaka, reli hiyo pia itakuwa na njia za chini tano, Uraloglu alisema. Aliongeza kuwa fedha za nje dola bilioni 2.79 zimepatikana kupitia juhudi zilizoongozwa na Wizara ya Fedha ya Uturuki.
Tangazo hilo linakuja siku chache baada ya mkutano wa utatu katika Ikulu ya Marekani, ambapo Rais wa Azerbaijan İlham Aliyev, Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan, na Rais wa Marekani Donald Trump walitia saini azimio la pamoja.
Makubaliano hayo yana lengo la kumaliza miongo kadhaa ya mgogoro kati ya Armenia na Azerbaijan, wakiahidi kumaliza mapigano, kurudisha uhusiano, na kufungua njia za usafiri — ikiwemo ushoroba wa Zangezur.
Njia hiyo imesababisha wasiwasi nchini Iran, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipinga mradi huo, unaoonekana kulenga kupunguza ushawishi wa Iran kwa Armenia.
Siku ya Jumatatu, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alisafiri hadi jijini Yerevan kwa mazungumzo na viongozi wa Armenia na pia kuzungumza kuhusu njia.
Wachanganuzi wanasema mradi huo wa reli, ukiunganishwa pamoja na azimio la amani la hivi karibuni, unaweza kubadilisha mfumo wa biashara na usafiri katika eneo hilo la mataifa ya Caucasus ya Kusini.