Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.1 kwa kipimo cha Richter lilitokea Sindirgi, magharibi mwa Uturuki, siku ya Jumapili, kama ilivyoripotiwa na shirika la usimamizi wa maafa la Türkiye (AFAD).
Tetemeko hilo lilihisiwa katika miji kadhaa ya magharibi mwa nchi hiyo, ikiwemo Istanbul na eneo maarufu la watalii la Izmir. Hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Takriban majengo 10 yalianguka huko Sindirgi, kitovu cha tetemeko hilo, yakiwemo jengo la ghorofa tatu katikati ya mji, kama alivyotangaza Meya Serkan Sak kupitia vyombo vya habari vya ndani vya Türkiye.
"Watu sita waliishi katika jengo hili la ghorofa tatu. Wanne wameokolewa kutoka kwenye kifusi," alisema, akiongeza kuwa juhudi za kuwaokoa wawili waliobaki zinaendelea.
"Majengo na misikiti imeharibiwa, lakini hatujapokea ripoti za kupoteza maisha," aliongeza.
Tetemeko hilo lilitokea saa 1653 GMT, na mitetemeko ya baadae ilikuwa na ukubwa wa kati ya 3.5 hadi 4.6 kwa kipimo cha Richter, kulingana na taarifa za AFAD.
Uturuki imegawanyika na mistari kadhaa ya kijiolojia ya ufa, ambayo hapo awali imesababisha majanga makubwa nchini humo.
Matetemeko mawili ya ardhi mnamo Februari 2023 katika eneo la kusini-magharibi yaliua angalau watu 53,000 na kuharibu Antakya, eneo la mji wa kale wa Antiokia.
Mwanzoni mwa Julai, tetemeko la ukubwa wa 5.8 katika eneo hilo hilo lilisababisha kifo kimoja na kuwajeruhi watu 69.