Jamii hiyo ya Wangazija ambayo imekuwepo katika maeneo ya Mombasa kwa muda mrefu, haijatambuliwa kama moja ya makabila nchini Kenya, licha ya mchango wake kihistoria.
“Hawa Wangazija wanazungumza Kiswahili na wanaishi katika maeneo ya pwani ya Kenya, hasa katika kaunti ya Mombasa. Licha mchango wake wa kitamaduni na kidini katika eneo hilo, bado wanaendelea kutengwa,” alisema Seneta Faki.
Kulingana na Faki, kutotambua jamii hiyo rasmi kunawanyima fursa ya kupata huduma muhimu za serikali, na uwakilishi katika taasisi za umma pamoja na kujumuishwa katika mipango mikakati ya kuimarisha maisha ya jamii ndogo ndogo.
Faki anasema hili ni kinyume na katiba ambayo inahimiza usawa na kujumuisha watu.
Ametaka kufahamu kama kuna hatua zozote zinazoangaziwa na taasisi za serikali katika kuwatambua rasmi watu wa jamii ya Wangazija.
Seneta huyo wa kaunti ya Mombasa pia anataka jamii hiyo ijumuishwe katika sensa za kitaifa, uteuzi wa nafasi za umma na miradi ya maendeleo inayolenga jamii zilizotengwa.
Asili ya Wangazija ni kutoka katika visiwa vya Comoro.