Maelfu ya watu katika mji wa Sawakin nchini Sudan wamefanya mkutano mkubwa wa hadhara kuonyesha shukrani kwa Uturuki na watu wake kwa msaada wao wakati wa changamoto kubwa nchini Sudan.
Uturuki imekuwa ikisaidia Sudan kwa misaada ya kibinadamu na juhudi za kutatua vita vinavyoendelea nchini humo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na maafisa wa Ubalozi wa Uturuki, akiwemo Balozi Fatih Yildiz. Ubalozi wa Uturuki nchini Sudan ulionyesha shukrani kwa mkusanyiko huo wa "Asante Uturuki, Asante Erdoğan".
Nchi hizi mbili "zitaendelea kusimama pamoja, kama tulivyofanya kwa karne nyingi," iliongeza katika chapisho kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii X.
Sudan imekuwa ikikumbwa na vita vikali tangu Aprili 2023 kati ya jeshi na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kufuatia mvutano wa mpito kuelekea utawala wa kiraia.
Zaidi ya watu 24,000 wameuawa na mamilioni wengine wamepoteza makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya mashirika ya Uturuki, yakiwemo Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uturuki, TIKA, yamekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada wa kibinadamu kwa waathirika.