Serikali ya Kenya imepuuza tishio kwamba Marekani huenda ikafuta uhusiano wake wa Karibu na nchi hiyo.
Hio ni kufuatia ripoti kuwa seneta mmoj wa Marekani amependekeza Marekani ichunguze na kutathmini uhusiano wake na Kenya.
Waziri Mkuu wa Kenya Musalia Mudavadi amethibitisha haya wakati muswada unaopendekezwa katika Seneti ya Marekani ukitishia kufuta hadhi ya nchi hiyo isiyo ya NATO (MNNA) kufuatia uhusiano wake wa kibiashara na Iran na Urusi.
Akizungumza na wabunge siku ya Alhamisi, Musalia alipuuza madai kwamba uhusiano wa kidiplomasia wa Kenya na Tehran na Moscow ulikuwa wa hatari.
“Tuna uhusiano na Iran kwa sababu ni wanunuzi wakubwa wa chai yetu. Kama serikali tuna jukumu la kutafuta soko kwa wakulima wetu wa chai, lazima tuuze kahawa, na maua yetu. kwa hiyo lazima kutafuta soko,” Mudavadi amesema.
Alisisitiza kuwa taifa lilikuwa linatumia tu haki yake kuu ya kutafuta fursa za kiuchumi kwa wakulima na wafanyabiashara wake.
"Kuna upotoshaji kuhusu baadhi ya masuala haya," aliiambia Kamati ya bunge.
"Kenya ni nchi huru na lazima iwe huru kushirikiana na taifa lolote kwa maslahi ya watu wake," CS alisisitiza.
Mfumo wa Marekani wa biashara na nchi nyengine unaoitwa AGOA unafikia kikomo mwaka huu 2025, na haijulikani ikiwa Marekani itaendelea nayo.
“AGOA inakaribia kufikia mwisho na ilikuwa motisha iliyotolewa na Marekani kwa nchi zote za Afrika sio Kenya tu, hivyo ikiwa Marekani haitafanya upya mkataba wake na nchi zote za Afrika basi lazima kila nchi ifanye majadiliano ya moja kwa moja na Marekani,” amesema huku akielezea kuwa tayari kupitia Wizara ya Biashara Kenya inafanya majadiliano na Marekani kuhusu biashara.
Kenya ni kati ya nchi ambazo serikali ya Rais Donald Trump imetoza ushuru kwa bidhaa kutoka kwake.
“Kuna maongezi mengi tunayofanya na Marekani kama changamoto ya ushuru mpya kwa bidhaa zetu. Lakini Kenya imepata ushuru ya chini zaidi ambayo ni asilimia 10. Kuna nchi nyengine Afrika na kimataifa zillizopewa ushuru zaidi ,” aliongezea.