Serikali ya Somalia ilisema kuwa imewasimamisha kazi na kuwaweka kizuizini wanachama kadhaa wa kikosi cha makomandoo waliofunzwa na Marekani kwa kuiba mgao uliotolewa na Marekani, na kuongeza kuwa inachukua jukumu la kutoa mgao wa jeshi hilo.
Kitengo cha Danab kimekuwa nguzo muhimu ya juhudi zinazoungwa mkono na Marekani kupambana na kundi la wanamgambo wa al Shabaab wenye mafungamano na al Qaeda. Marekani ilikubali mwezi Februari kutumia zaidi ya dola milioni 100 kujenga hadi vituo vitano vya kijeshi vya Danab.
Afisa mmoja wa Marekani alisema katika taarifa yake kwa Reuters kwamba Washington inachukulia kwa uzito tuhuma zote za ufisadi.
"Tunatazamia kushirikiana na Danab katika kuunda ulinzi unaohitajika na hatua za uwajibikaji ili kuzuia matukio yajayo ambayo yanaweza kuathiri usaidizi wa siku zijazo," afisa huyo alisema, bila kuzungumzia moja kwa moja iwapo usaidizi wowote wa Marekani ulikuwa tayari umesimamishwa.
Wizara ya ulinzi ya Somalia ilisema katika taarifa yake mwishoni mwa Alhamisi kwamba imewaarifu washirika wa kimataifa kuhusu wizi huo na itashiriki matokeo ya uchunguzi wake.
Marekani ilikubali mwaka 2017 kusaidia kutoa mafunzo na kuandaa kikocsi cha Danab chenye askari 3,000 kufanya kama kikosi cha mashambulizi ya haraka dhidi ya al Shabaab. Kundi hilo limekuwa likiendesha uasi dhidi ya serikali kuu tangu 2006.
Danab amekuwa ikishirikiana katika mashambulizi ya kijeshi na wanajeshi wa Somalia na wanamgambo wa koo washirika tangu 2022 ambayo awali ilifanikiwa kunyakua maeneo mengi kutoka kwa al Shabaab katikati mwa Somalia.